Update:

WANAFUNZI WA SHULE ZA ARUSHA IKIWEMO WINNING SPIRIT WAPEWA ELIMU YA MADINI


Mkufunzi kutoka Taasisi ya Gemological Institute of America (GIA), Elizabeth Bokaba, akiwafundisha elimu ya Jemolojia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Winning Spirit 

Jumla ya Wanafunzi 30 kutoka Shule za Sekondari za Arusha Day na  Wining Spirit wenye umri kati ya miaka 12- 15 wamepatiwa
mafunzo ya Jemolojia katika Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito
yanayoendelea jijini Arusha.


Mafunzo hayo yanayojulikana kama GemKids yametolewa na Wakufunzi kutoka
Taasisi ya Gemological Institute of America (GIA) na kuratibiwa na Kituo
cha Jimolojia Tanzania Cha Arusha, (TGC).

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Mratibu wa TGC, Erick Mpesa amesema kuwa,
mafunzo hayo ya Jemolojia, yanalenga kuwapa ufahamu wanafunzi ili kuwa
na uelewa wa madini ya vito, kujua matumizi yake, kuyatumia na baadaye
kuwawezesha kuingia katika biashara ya madini huku wakiwa na uelewa
mzuri na rasilimali hizo ambazo zinapatikana katika maeneo mbalimbali
nchini.


Akizungumzia mahusiano ya TGC na Taasisi ya GIA, Mpesa amesema kuwa, TGC imelenga
kuendeleza ushirikiano na Taasisi hiyo kwa siku za baadaye hususani
katika masuala ya utafiti na mafunzo na kuongeza kuwa, uhusiano uliopo
baina ya taasisi hizo, umewezesha baadhi ya watumishi wa kituo hicho
kupata mafunzo katika taasisi hiyo.

Kuhusu mpango wa TGC kutoa mafunzo kwa Watanzania, alisema kuwa, tayari
kupitia Maonesho ya Vito ya Arusha, kituo hicho kuanzia mwaka 2014
kimetoa mafunzo ya ukataji na unga'rishaji wa madini ya vito kwa jumla
wanawake 47 na kueleza kuwa, hivi sasa jumla ya wanawake 18 wanaendelea
na mafunzo hayo na wanatarajiwa kuhitimu ifikapo tarehe 19 ya mwezi
huu.

"Kutokana na changamoto ya ajira wahitimu wetu tunawashauri kujiunga katika
vikundi ili kuwawezesha kupata ruzuku pale zinapotolewa na Serikali. Hii
inawezesha rasilimali inayotumika kuwafundisha kuwawezesha vijana hawa
isipotee bure. Lengo letu ni kuwawezesha waweze kujiajiri na kuajiriwa,"
alisisitiza Mpesa.

Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Vito ya Arusha yalianza rasmi tarehe 3 Mei na yanataajiwa kufungwa tarehe 5 Mei,2017.

Wanafunzi wa Shule wa Sekondari ya Winning Spirit  wakimsikiliza Mkufunzi kutoka Taasisi ya Gemological Insitute of America (GIA) , Elizabeth Bokaba (hayupo pichani). Wanafunzi hao wamepata mafunzo kuhusu mafunzo ya Jimolojia.

No comments