Update:

Wakenya watakakiwa kudumisha amani wakati na baada ya uchaguzi

Wakenya wametakiwa kudumisha amani wakati huu wa harakati za kampeni za uchaguzi na hata baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Agosti.

Wakiongea kwenye hafla ya kuzindua mpango wa usalama wakati wa uchaguzi huo Inspekta wa polisi nchini Kenya Joseph Boinnet na mwenyekiti wa tume ya maridhiano na uwiano wa kitaifa Francis Kaparo wametoa onyo kwamba wale wakataojihusisha na ghasia ama uchochezi watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Huku ikiwa imesalia miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya, vyombo husika vya usalama, uchaguzi na mshikamano wa kitaifa vimezindua mpango wa kiusalama na kueleza utayari wao kwenye zoezi hilo la Agosti 8.
Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Wafula Chebukati anasema wameweka mipango ya kutosha kuendesha zoezi hilo.
“Kama tume tuko tayari kuendesha uchaguzi wa huru na wa haki ifikapo agosti 8 mwaka huu. Tuna fahari kuongoza na kutekeleza jukumu hili la kitaifa na tunashirikiana na wadau wengine kama vile ofisi ya kiongozi wa mashtaka, huduma ya kitaifa ya polisi, ofisi ya mkuu wa sheria na shirika la umoja wa mataifa la maendeleo UNDP. Kama tume pia tutahakikisha tumeweka mikakati ya kuwa na haki kwenye mchakati wote wa uchaguzi. Pia tunajiandaa kukabili kithabiti vitishio vyote vya ghasia vinavyoweza kutokea”
Tayari tume hiyo imewasajili zaidi ya wapiga kura milioni 14.3 na pia wakenya waihio Uganda, Tanzania, Burundi, Rwanda na Afrika Kusini wameandikishwa kushiriki upigaji kura.
Lakini wakati wakilisubiri kwa hamu zoezi hilo, matukio ya ghasia za baada ya uchaguzi mwaka wa 2008 ni swala nyeti ambalo polisi wanajiandaa kulikabili iwapo litatokea.
Inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinet kwenye mkutano wa Jumanne amewaonya wanasiasa dhidi ya ghasia wakati wa kampeni, uchaguzi, na baada ya uchaguzi akisema bila kujali misingi ya vyama ama hadhi yeyote atakaye jihusisha na uvujaji wa sheria atachukuliwa hatua kali.
“Kwa upande wetu tuko imara na tuko tayari kushiriki kwenye zoezi hili na tuko tayari kutoa maafisa wote wa polisi wanaohitajika, na pia tumefanya mipango husika na mashirika mengine ya kiusalama ili watupe majina ya maafisa wa polisi tutakaowateua kama polisi maalum kushiriki kwenye zoezi hili. Kwtu sisi jukumu letu ni kuweka mazingira yanayofaa kuwezesha wakenya kutekeleza haki yao ya kidemokrasia. Tutafuata sheria kama ilivyo na hatutakubali yeyote kutishia usalama”
Tayari serikali inawapatia mafunzo askari polisi zaidi ya 85,000 kwa ajili ya kulinda amani na utulivu kuhakikisha mchakato wote wa uchaguzi wa Agost 8 unaendeshwa kwa amani.
Hata ingawa polisi wanakaa macho kulinda usalama, lakini mwenyekiti wa tume ya maridhiano na uwiano wa kitaifa Francis Ole Kaparo anasema jukumu la kudumisha amani hasa ni la wanasiasa na wananchi.
“Nawaomba wakenya, kwamba hata ingawa polisi watafanya bidii kuhakikisha kuwa hakuna ghasia, nawaomba mfanye kampeni kwa njia ifaayo. Wapeni nafasi viongozi waeleze sera zao bila matusi na vitisho. Na wanasiasa wapeni wakenya nafasi ya kuishi na kuwachagua ”
Kwenye uchaguzi huo wapigakura watamchaguwa rais, naibu wake, wabunge (wawakilishi na maseneta) pamoja na wajumbe wa serikali za ugatuzi (magavana wa kaunti na wawakilishi wa tarafa).

No comments