Update:

UNICEF: Watoto laki 3 wakimbia nchi zao bila usimamizi wa yeyote


Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema watoto zaidi ya laki tatu kote duniani aghalabu yao wakitokea nchi za Afrika wamelazika kuwa wakimbizi na wahajiri pasina usimamizi wa mtu yeyote katika muda wa miaka miwili iliyopita.

UNICEF imesema asilimia 92 ya watoto waliowasili barani Ulaya tokea mwaka jana 2016 hadi mwanzoni mwa mwaka huu hawakuwa na wazazi wala wasimamizi huku baadhi yao wakilazimika kutengana na wazazi wao katika safari za kutisha za baharini.

Justin Forsyth, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF amesema mamia ya watoto wamepoteza maisha katika ajali za boti wakijaribu kuelekea barani Ulaya kupitia Italia, na kwamba akthari yao wanatokea nchi za Eritrea, Gambia, Nigeria, Misri na Guinea.Baadhi ya nchi za Ulaya zinawatenganisha wahajiri watoto na wazazi wao

Amesema wengi wa watoto hao wanajikuta katika mtego wa biashara ya magendo ya binadamu na wanapofika barani Ulaya wanalazimishwa kuingilia ukahaba wakiwa na umri mdogo.

Wahajiri zaidi ya 45,000 wamewasili Italia kwa boti hafifu za plastiki wakitokea kaskazini mwa Afrika tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa huku wengine zaidi ya 1,222 wakiaga dunia kwa kuzama baharini, hili likiwa ni ongezeko la asilimia 40 ya vifo vya wahajiri wanaoelekea Italia, ikilinganishwa na mwaka jana 2016.

Kwa mujibu wa Shirika la Uhamiaji Dunia IOM, zaidi ya wahajiri 5,000 walifariki dunia katika Bahari ya Mediterranean mwaka uliomalizika wa 2016 katika jitihada za kuingia barani Ulaya

No comments