Update:

Sababu za kimsingi za umasikini wa watoto katika Mashariki ya Kati

Utafiti uliofanywa na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF katika nchi 11 za Mashariki ya Kati unaonyesha kuwa, kwa akali watoto milioni 29 ambao ni robo ya watoto wote wa eneo hili wanaishi katika umasikini.
Utafiti huo wa UNICEF unaonyesha kuwa, watoto hao hawapati huduma muhimu za kimsingi za maisha kama vile elimu, tiba, nyumba zinazofaa kwa makazi, chakula na maji safi na salama ya kunywa.
Moja ya malengo muhimu kabisa ya Milenia ya Umoja wa Mataifa ni ustawi wa kudumu. Aidha moja ya nguzo muhimu za kupatikana ustawi wa kudumu ni kupambana na umasikini na njaa duniani. Hii ni katika hali ambayo, katika kipindi cha miaka 17 iliyopita, tangu kuanza Milenia mpya, si tu kwamba, hali ya umasikini na njaa ulimwenguni haijapungua, bali hali hiyo imezidi kuwa mbaya siku baada ya siku hususan katika maeneo ya Mashariki ya Kati na barani Afrika, hali ambayo haiwezi kulinganishwa kabisa na maeneo mengine duniani. 

Watoto wa Yemen wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa na magonjwa

Swali ni kwamba je, ni kwa nini katika eneo la Mashariki ya Kati kuna robo ya watoto ambao wanaishi katika umasikini? Hapana shaka kuwa, jibu la swali hili ni kwamba, hali ya eneo la Mashariki ya Kati inatokana na sababu za nje. Kwa maneno mengine ni kuwa, muundo wa Mashariki ya Kati hautokani na matukio ya ndani bali ni mambo ya kisiasa yaliyopandikizwa kutoka nje na madola makubwa ya kisiasa hususan Marekani na Uingereza. 
Muundo huo uko kwa namna ambayo kwa mujibu wa Barry Buzan mwananadharia wa mahusiano ya kimataifa anasema katika madhumuni ya maneno yake kwamba, mivutano ya eneo hili ni ya kupandikizwa. Kwa hakika hii leo, uingiliaji wa madola makubwa ya Magharibi katika masuala ya ndani ya Mashariki ya Kati ni moja ya sababu za kukosekana amani na uthabiti katika eneo hili.
Vita  ambavyo hii leo vimebadilisha utambulisho wake katika Mashariki ya Kati kutoka baina ya nchi na nchi  na kuhamia ndani ya nchi, ni matokeo ya sera za madola ya Magharibi.

Watoto wa Gaza , Palestina ni miongoni mwa watoto wanaoteseka kutokana na mzingiro wa Israel dhidi ya eneo hilo

Kwa maneno mengi ni kama anavyoamini Samuel P. Huntington mwananadharia wa Kimarekani kwamba, vita baina ya tamaduni mbalimbali vimegeuka na kuwa vita vya ndani ya tamaduni. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, sababu hiyo ndio iliyopelekea kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya watoto na matokeo yake ni watoto kukabiliwa na njaa, umasikini na kulazimika kuwa wakimbizi.
Moja ya sababu za uingiliaji wa madola ya Magharibi katika Mashariki ya Kati ni hii kwamba, aghalabu ya tawala za eneo hili si tu kwamba, hazijitemegei, bali zimepatikana kutokana na siasa za Kimagharibi. Hii leo pia kubakia madarakani tawala hizo kunategemea himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi. 
Natija ya uingiliaji wa madola ya Magharibi na kutiwa saini mikataba ya kiusalama baina ya watawala wa Kiarabu na Wamagharibi kumeifanya hali ya kutoaminiana baina ya nchi za eneo kufikia katika kiwango cha hali ya juu kabisa. Hii ni katika hali ambayo, moja ya masharti ya mwanzo ya kupatikana amani na uthabiti katika eneo ni kutawala anga ya kuaminiana katika uhusiano wa nchi za eneo.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF

Kutawala anga ya kutoaminiana katika uhusiano baina ya nchi mbalimbali huwa sababu ya kuongezeka gharama za kijeshi. Lakini kuweko anga ya kuaminiana katika mahusiano baina ya nchi mbalimbali huwa sababu ya kwamba, badala ya kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua silaha na zana za kivita, fedha hizo hutumika katika masuala ya huduma kwa wananchi na hivyo kupunguza kiwango cha umasikini na njaa. 
Hii leo kuweko anga ya kutoamiana nchi mbalimbali kumelifanya eneo la Mashariki ya Katii kugeuka na kuwa soko la kuuzia silaha. Katika mazingira kama haya, umasikini na njaa si tu kwamba, havitapungua bali mwenendo wa kuongezeka kwake utaendelea kushuhudiwa siku baada ya siku.

No comments