Update:

Naibu Waziri wa Habari hatambui ukamatwaji wa waandishi

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura amesema kuwa hana taarifa kuhusu waandishi wa habari kukamatwa na polisi au viongozi mbalimbali wa Serikali na kuzuiwa kutimiza majukumu yao ya kazi. Wambura alikua akijibu swali bungeni lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum(Chadema), Devotha Minja aliyeuliza msimamo wa Serikali kuhusu matukio ya uvamizi kwa waandishi wa habari wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi. "Mimi ndio kwanza nasikia kutoka kwako mheshimiwa Mbunge, naomba baada ya kutoka hapa tuonane ili unipatie taarifa kwa kina kuhusu hayo matukio ya kukamatwa waandishi au kuzuiwa kutimiza majukumu yao ya kazi,’ alisema Wambura. Minja alihoji swali bungeni akisema hivi karibuni kumekuwa na matukio ya kushambuliwa waandishi wa habari wakiwa kazini ikiwa ni pamoja na tukio la mkuu wa mkoa kuvamia studio za kituo cha televisheni cha Clouds na pia tukio la waandishi wa habari kuvamiwa wakiwa katika kukusanya habari katika mkutano wa CUF eneo la Mabibo. Minja pia alihusisha tukio la jana la waandishi wa habari wa vituo mbalimbali vya habari Arusha kukamatwa na polisi wakiunganishwa na Meya wa Arusha, Calist Lazaro na wamiliki wa shule binafsi, walipokua wakitoa salamu za rambirambi katika Shule ya Lucky Vincent ambayo ilipoteza watu 35 ikiwa ni wanafunzi , walimu na dereva waliopoteza maisha katika ajali ya basi huko Karatu hivi karibuni.

No comments