Update:

Mongella aongoza ung’oaji na uteketezaji wa bangi tani 15


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella leo ameiongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo kung’oa na kuteketeza zaidi ya tani 15 za bangi iliyolimwa ndani ya eneo la hifadhi ya msitu wa Buhindu Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema. Kazi hiyo haikuwa rahisi kwani wajumbe wa kamati hiyo, mgambo wa halmashauri, waandishi wa habari na watu wengine waliokuwemo kwenye msafara huo walilazimika kutembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa 25 kutoka kijiji cha Ilyamchele, Kata ya Kazunzu hadi kufikia shamba hilo lenye ukubwa wa ekari nne. Mhifadhi wa msitu huo, Hamad Ali amesema hilo ni tukio la pili tangu Februari, mwaka huu kwa vyombo vya dola kung’oa na kuteketeza bangi eneo hilo. Katika tukio la kwanza, zaidi ya ekari 10 ziliteketezwa.