Update:

Ijuwe Mbinu Mpya Ya Kuongeza Ufanisi Na Uzalishaji katika maisha ya kila siku

Image result for matumizi ya muda
Imeandikwa na Kocha
Asante sana kwa kuendelea kuwa na mimi kila siku, tukijifunza kwa pamoja na kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi. Nimekuwa najifunza vitu vingi kwenye maisha, na kila ninachojifunza nakijaribu kwenye maisha yangu na kuona matokeo yake mazuri. Na kila kinachokuwa na matokeo mazuri, siachi kukushirikisha wewe rafiki yangu, ili na wewe uweze kunufaika na maarifa na mbinu mbalimbali za kuhakikisha tunakuwa na maisha bora.
Moja ya changamoto kubwa za kufanya kazi yenye ufanisi na kwa kiwango kikubwa zama hizi ni kelele. Na ubaya wa kelele ni kwamba tunatembea nazo popote pale ambapo tupo, kwa mfumo wa simu zetu za mkononi ambazo zinajulikana kama ‘smartphone’. Simu hizi zimekuwa kelele kwetu kwa sababu tunatembea na dunia nzima kwenye kiganja cha mkono. Jambo lolote litakalotokea duniani, unalipata wakati huo huo. Wanakuambia ni mubashara yani. Sasa ni vigumu sana kuweza kufanya kazi yenye maana, inayohitaji akili yako itulie na kufikiri kwa kina, iwapo kelele hizi zitakuwa zinakuingilia kila mara.
Ile umefanya kazi kidogo, mara ujumbe kwenye simu umeingia, unaacha na kuusoma, ukija kurudi kwenye kazi yako, unakuwa umerudi nyuma sana, mpaka uje tena kufikia pale ulipokuwa, inakuchukua muda. Hapo bado hujaingia kwenye mitandao ya kijamii kuangalia nini kinaendelea, hujaenda kwenye whatsap kuona yanayoendelea. Na bado hujaingia kwenye email, hujasoma magazeti, hujasikiliza redio, hujaangalia tv. Zote hizi ni kelele ambazo hazitakuachia ufikiri kwa uhuru na kuzalisha kazi bora kabisa.
Katika kutafuta njia ya kuweza kupunguza kelele hizi ili kuweza kufanya kazi bora, ndipo nilikutana na mbinu hii inayoitwa MONK MODE MORNING.
Katika mbinu hii, unailinda sana asubuhi yako na kuhakikisha haiingiliwi na kelele zozote. Unachofanya ni wewe kutuliza akili yako na kuipeleka kwenye uzalishaji wa kile muhimu ambacho umepanga kufanya. Hivyo kila asubuhi, unatenga muda wako wa kufanya kazi, ambao hautaingiliwa na mtu yeyote yule.
Katika muda huo haupo kwenye mtandao, wala hupokei na kujibu simu wala ujumbe unaotumiwa. Wewe unaiweka akili yako kwenye kufanya kazi, unaikamua hasa na hapo ndipo unaweza kuzalisha kazi iliyobora.
Ukifuatilia watu wengi ambao wameweza kufanya makubwa, iwe ni kwenye sayansi  na teknolojia, kwenye uandishi na hata kwenye uongozi, wamekuwa na muda wao peke yao, muda ambao wanafanya kazi ya kufikiri kwa kina, muda ambao hawana usumbufu wowote ule. Ni katika muda huo ndiyo wanapata majibu ya matatizo yanayowasumbua kwa muda mrefu, wanakuja na uvumbuzi ambao unawasaidia wengi na hata kuja na mbinu bora zinazowasaidia watu.
Kwa upande wangu, ninategemea kupata masaa 6 mpaka nane kila asubuhi ya kufanya kazi bila kusumbuliwa kwa namna yoyote ile. Kwa kawaida, na mara nyingi nimekuwa naamka saa 10 asubuhi, hivyo kuanzia muda huo mpaka saa sita mchana sitakuwa napatikana kwa namna yoyote ile, bali muda huu nitaupeleka kwenye kazi zangu. Pia nafikiria kuanza mapema zaidi, labda saa tisa au saa tisa na nusu na kwenda mpaka saa tatu au saa nne. Nimejipa mwezi huu wa tano kwa majaribio ya hili, hivyo nitaona njia ipi itakuwa bora zaidi kwangu.
Zipo kazi nyingi ambazo nahitaji kuzifanya, yapo mawazo mengi ya kuboresha zaidi kazi zangu ambayo nimekuwa nayo kwa muda mrefu, nitayafanyia kazi kwenye kipindi hichi. 
Kama unahitaji kupata angalau muda wa kufanya kazi zako ambao husumbuliwi, nakushauri ujaribu mbinu hii. Siyo lazima utangaze kuifanya, bali jipe tu siku 30 za kuijaribu kisha ona matokeo yake yatakuwaje. Pia siyo lazima uijaribu kwa masaa mengi kama yangu, badala yake weka masaa yatakayoendana na mazingira yako ya kile unachofanya. unaweza kutenga masaa mawili, matatu na hata kuendelea. Ila nakushauri sana isiwe chini ya masaa mawili.
Kama ukichagua masaa mawili, basi hakikisha unaipanga asubuhi yako iweze kukupa masaa mawili ya kufanya kazi yako kabla ratiba zako za kawaida hazijaanza.
Kipimo pekee cha maisha yetu, ni namna ambavyo tunatumia muda wetu. Na matumizi ya muda wetu yamegawanyika kwenye makundi mawili. Kuna kula na kuzalisha. Watu wengi sana wanatumia muda wao kula, na simaanishi kula chakula, bali kula vitu vya wengine, mfano kusoma, kuangalia tv, kufuatilia mitandao ya kijamii na kadhalika. Lakini wachache sana ndiyo wanaozalisha, wanaotumia muda wao kufanya vitu ambavyo wengine wanavifuatilia. Nakushauri sana rafiki yangu, tumia wastani wa 2;1 kwenye muda wako kati ya kuzalisha na kula. Tumia mara mbili ya muda wa kula kuzalisha. Zalisha zaidi ya unavyokula. Wanaoleta mabadiliko duniani siyo walaji, bali wazalishaji. Zalisha, weka kazi, unda kitu, toa huduma, chora, imba, andika, ongea. Vyovyote vile, toa kitu ambacho kitafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

No comments