Update:

IFAHAMU SIRI YA UKWELI NA FAIDA ZAKE KATIKA MAISHA YAKO

Image result for ukweli

Karibu kwenye makala ya leo ya falsafa mpya ya maisha, ambapo tunakwenda kujenga falsafa mpya ya maisha ambayo inatuwezesha kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. Na kwa kuwa maisha ni kile mtu unachochagua, kupitia falsafa hii mpya tunaweza kuchagua kile kilicho bora kabisa. Wengine wanalazimika kuchagua kile kinachofanywa na wengi, ambacho mara nyingi siyo bora, sisi tunachagua kilicho bora kwa sababu tunajua.
Kwenye makala yetu ya leo ya falsafa mpya ya maisha tunakwenda kuangalia kuhusu ukweli. Tumeshajifunza sana umuhimu wa ukweli kwenye maisha na namna gani kutafuta ukweli kwenye kila jambo kunatuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwenye kila eneo la maisha letu.
Lakini lipo jambo moja la kusikitisha kuhusu ukweli, jambo hilo ni kwamba ukweli siyo kipaumbele cha binadamu. Yaani siyo kitu cha kwanza ambacho mtu atakimbilia anapohitaji kufanya maamuzi. Na hii inafanya ukweli uwe muhimu zaidi kwa kila mtu, kwa sababu kwa kuupenda na kuujua, unakuweka mbali na wengi wanaofanya makosa.
Watu hawapendi ukweli, bali watu wanapenda kitu wanachoweza kukiamini, hata kama ni kwa wakati. Hivyo wakiwekewa ukweli na imani, watakwenda na imani, hata kama imani hiyo hawana uhakika nayo, hata kama wamepandikizwa tu. Na hii ndiyo imekuwa inapelekea watu wengi kufuata kundi. Unakuta watu wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya lakini hawajui kwa nini wanafanya. Hawajawahi kukaa chini na kudadisi kwa kina kwa nini wanafanya kile wanachofanya.
Ukweli ni mgumu, ukweli unaumiza na ukweli haubembelezi. Sasa hilo linawafanya wengi kukimbilia kile rahisi kuamini, na siyo kile kigumu kufikiri kwa kina na kupata majibu sahihi. Ukijichunguza wewe mwenyewe kwa nini unaamini baadhi ya vitu unavyoamini, hutakuwa na majibu, lakini unaamini na kufanya, kwa sababu ndiyo umekuwa unafanya na ndivyo wengine wanavyofanya.
Ukweli pia umekuwa siyo kipaumbele cha wengi, kwa sababu wale wachache wanaoujua hawapendi wengine nao waujue. Wachache wanaujua ukweli na kuona nguvu yake, na hivyo kuhakikisha wengine hawaujui ili waendelee kuwatumia. Ndiyo maana tangu enzi na enzi, tawala zote zimekuwa zinawazuia watu kuujua ukweli. Watu wanapewa mambo rahisi kufikiria na kuongelea, na hivyo wanashindwa kuchimba na kujua ukweli.
Kazi yetu kama wanafalsafa ni kuujua ukweli na kuuishi, kazi ambayo siyo rahisi kwa sababu ya wengi wanaotuzunguka kutokutaka ukweli. Na hata wanafalsafa wa zamani, mambo hayakuwa rahisi kwao, kwa sababu wengi waliishia kufungwa na kuuawa kwa kufungwa kwa tuhuma za kuwaharibu vijana. Yaani vitendo vyao vya kuwafundisha watu ukweli, vilichukuliwa kama kuwaharibu wale waliokuwa wakiwafundisha.
Sasa hivi adhabu ya kuujua ukweli inaweza isiwe kubwa kama ya kufungwa au kuuawa, bali adhabu ni kutengwa na kundi la wengi. Pale unapochagua kusimamia ukweli, utatengwa na kundi la wengi, ambao wao watachagua kile ambacho wengi wamechagua, ambacho mara nyingi siyo ukweli. Watakuona wewe ndiye msaliti, wewe ndiye uliyepotea na wewe ndiye usiyejua ukweli. Hivyo sisi wanafalsafa lazima tujue hii ni adhabu ya kuishi falsafa na tusiichukulie kama adhabu, kwa sababu pamoja na kutengwa huku, mwisho wa siku sisi tutashinda. Ukweli haujawahi kushindwa hata mara moja, ni swala la muda tu.
Hivyo kama utaweza kusimamia ukweli wakati wote, lazima mwisho utaibuka na ushindi. Ukweli ni kitu adimu na kigumu kusimamia kwenye zama hizi, na hivyo inatufanya sisi wanafalsafa tuuthamini zaidi na kuuishi zaidi. Popote unapokuwa, tafuta kuujua ukweli. Wakati wengi wanakubaliana na maelezo rahisi yanayotolewa, wewe chimba ndani zaidi, hoji zaidi, dadisi zaidi na ukweli utauona. Ila nikupe tahadhari, mara nyingi ukweli hautakuwa unavyotaka wewe, utaweza kukuumiza zaidi, lakini kama mwanafalsafa makini, lazima uweze kuishi na hilo.
Ukweli ndiyo nguzo kuu ya falsafa, na hakuna mtu yeyote anayeweza kuficha ukweli. Na uzuri zaidi, hakuna anayemiliki ukweli, ukweli ni wa wote na unapatikana bure. Ni juhudi zetu sisi wanafalsafa kuutafuta ukweli na kuuishi ili tuweze kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Imeandikwa na kocha

No comments