Update:

Aua mke kwa shoka, naye ajinyonga, mwingine aua mpenzi wake kwa panga


Mkazi wa Kijiji cha Msia wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, Patrick Kipesa (39) amejinyonga kwa kutumia kamba ya katani mara baada ya kuumua mkewe kwa kumkata kata na shoka sehemu mbalimbali za mwili wake. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Polycarp Urio amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 1:30 asubuhi katika Kijiji cha Msia wilayani Sumbawanga.
 Alimtaja aliyeuawa kuwa ni Theresia Selemani (49) mkazi wa kijiji cha Msia aliuawa kwa kukatwa katwa na shoka maeneo ya kichwani na shingoni na mume wake huyo.
Amesema baada ya tukio hilo mtuhumiwa naye alijiua kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani akiwa sebuleni kwake na kufariki papo hapo. Chanzo cha kufanya mauaji hayo na yeye kujiua ni wivu wa mapenzi baada ya mtuhumiwa kuhisi kuwa mkewe ana mahusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine, ambapo alimvizia marehemu na kumkata na shoka shingoni na kichwani.
Katika tukio nyingine lililotokea jana, msichana Fatuma Yusuph (22) mkazi wa mtaa wa Shengetela, aliuawa kwa kukatwa na panga kichwani na mzazi mwenzie.
 Inadaiwa kuwa kabla ya mauti kumfika msichana huyo, kulizuka ugomvi baina yake na mwenzi wake ambaye jina linahifadhiwa chanzo kikiwa ni wivu wa kimapenzi ndipo waliposhindwa kuelewana na mwanaume huyo kumjeruhi kwa kumkata na panga kichwani msichana huyo. Baada ya tukio hilo marehemu alifika katika kituo cha polisi kutoa taarifa ya kujeruhiwa akiwa na hali mbaya ambapo alipewa PF3 ili aende akatibiwe na ndipo mauti ilipomkuta akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa iliyopo mjini hapa. Taarifa za kipolisi zinaeleza kwamba baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia na kutoroka na kuelekea kusikojulikana.

No comments