Update:

Afariki dunia baada ya kukatwa sikio

Mkazi wa kijiji cha Maligisu Wilaya ya Kwimba, Mabindo Paul (33), amefariki dunia baada ya kukatwa sikioni. Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema tukio hilo lilitokea Mei 22 mwaka huu saa 2.00 usiku katika kitongoji cha Samirunga na sababu za mtuhumiwa kutenda kosa hilo hazijajulikana. Msangi amesema baada ya kukatwa sikio la upande wa kushoto, marehemu Mabindo alikimbilia nyumbani na kuwaleza ndugu zake kilichotokea ndipo wakamkimbiza katika kituo cha afya cha Maligisu lakini juhudi za kuokoa maisha yake zilishindikana. “Ndugu wa marehemu waliwahi kutoa taarifa kwa polisi ambapo msako ulifanikisha mtuhumiwa kutiwa mbaroni na mwili wa marehemu tayari umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi,” amesema Kamanda Msangi. Katika siku za hivi karibuni, Wilaya ya Kwimba imeshuhudia matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi baada ya wiki iliyopita mwanamke mmoja, Meja Ntende (35), mkazi wa kijiji cha Ibaya Kata ya Runele alidaiwa kumuua mumewe, Mbiye Nynda (45) kwa kumpia na fimbo kichwani.

No comments