Update:

5 wauawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu Somalia


Kwa akali watu wawili wameuawa na wengine watatu wamejeruhiwa katika mripuko wa bomu la kuendeshwa kutokea mbali katika viunga vya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Hayo yameelezwa na tovuti ya habari ya Garowe na kuongeza kuwa, basi la abiria jana Jumapili lilikanyaga bomu hilo lililokuwa limetengwa barabarani katika eneo la Garasbaley, yapata kilomita 9 magharibi mwa Mogadishu na kusababisha maafa hayo.

Mashuhuda wa mripuko huo wamesema kwamba, hujuma hiyo ilikuwa imelenga msafara wa magari ya jeshi ambao ulikuwa unapita katika eneo hilo. Habari zaidi zinasema kuwa, waliojeruhiwa katika shambulizi hilo akiwemo mwanamke mmoja wanatibiwa katika hospitali moja mjini Mogadishu.  Shambulio jingine la al-Shabaab mjini Mogadishu hivi karibuni

Hadi tunaenda mitamboni, hakuna kundi lololote lililokuwa limekiri kuhusika na hujuma hiyo ya bomu, ingawaje kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab ni maarufu kwa kufanya mashambulizi ya aina hii.

Magaidi wa al-Shabaab wamekuwa wakifanya mashambulizi dhidi ya misafara ya magari jeshi na Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM inayotumia barabara kuu ya Mogadishu kuelekea katika wilaya ya Afgoye na maeneo mengine ya nchi.

No comments