Update:

Upinzani Kenya wamteua mgombea wa urais


Vyama vya upinzani nchini Kenya ambavyo viko chini ya muungano wa National Super Alliance (NASA) vimemteua aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka huu.Siasa nchini humo vimepamba moto wakati ikiwa imesalia miezi 3 tu kabla ya uchaguzi huo.
Katika bustani ya Uhuru mjini Nairobi wafuasi wa muungano wa upinzani National Super Alliance (NASA) walifurika kuanzia saa kumi na mbili alhamis.
Ni siku muhimu ya kuzindua atayepeperusha bendera ya urais kwenye uchaguzi wa Agosti 8.
Baada ya masaa kadhaa hatimaye vigogo watano wenye vyama tanzu vya muungano huo wakafika tayari kumtangaza mmoja wao kuwa mgombea wa urais kushindana na chama tawala cha jubilee.
Kama ilivyokuwa imetabiriwa na wengi aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga alitangazwa mgombea na naibu wake wa rais atakuwa ni Kalonzo Musyoka.
Raila Odinga akihutubia wafuasi baada ya kukabidhiwa bendera anasema anachukua uteuzi huo kama heshima kubwa kutoka kwa wenzake.
"Leo hawa ndugu zao wamesema Raila tosha , ni heshima kubwa kwa hawa ndugu zao kwanifanya ni bebe bendera ya mwungano wa NASA katika mchwano ambao unakuja."
Na kwenye meza yao ni ahadi za kuboresha uchumi jira kwa vijana na kuwa na jamii inayostawi.
"Katika yetu sisi watu watano tunataka kubadilisha kenya ili tuweze kutekeleza ndoto ya taifa letu, vijana wetu waweze kupata kaz, gharama ya bidhaa ishuke, madaktri na walimu walipwe vizuri."
Kulingana na makubaliano yao, Musalia Mudavadi anayeongoza chama cha Amani National Congress atakuwa waziri mkuu mratibu wa shughuli za serikali huku naye kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula akiwa naibu waziri mkuu mratibu wa uchumi.
Naye kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto atakuwa naibu waziri mkuu atakayesimamia utawala na huduma za jamii.
Ni mara ya pili kwa Raila na Kalonzo kuwa kwenye muungano mmoja wa kugombea uongozi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta.
Kalonzo Musyoka anasema hawajali tena mamlaka lakini lengo lao ni kujitolea kwa ajili ya maendeleo na umoja wa kitaifa.
"Serikali tutakayo iunda itajumuisha kila mtu kwa sababu kenya ni kubwa kuliko mtu binafsi."
Lakini raia wana maoni tofauti kuhusu muungano wa NASA utakaongozwa na Odinga.
"Nimefurahi sana kwa sababu hiyo ndiyo ilikuwa maombi yangu, ufisadi sasa naona itaisha."
"Raila ni kiongozo ambaye ako na maono, na atabadilisha maisha ya wetu, na kutengeneza ajira kwa vijana."
Na huku ikiwa imesalia miezi mitatu kabla ya uchaguzi kufanyika siku zijazo zinatarajiwa kuwa na shughuli nyingi za kisiasa katika pande zote mbili za vyama vikuu yaani jubilee na NASA.

No comments