Update:

Familia yatengwa kutokana na Ugonjwa sugu wa ngozi


WAKAZI wa kitongoji cha Nkata kilichopo katika kijiji cha Kate, Kata ya Kate katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wameingiwa na hofu kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa ngozi, uliowakumba watu wanane wa familia moja kijijini humo.
Hayo yalibainika baada ya kufanya mazungumzo na Paroko wa Kanisa Katoliki, lililopo katika kata ya Kate, Padre Jofrey Kitaya ambaye alimwokota mtoto Peter Kazumba (13), aliyelala usiku kucha pembezoni mwa Zahanati ya Mtakatifu Anna, inayomilikiwa na Watawa wa Kanisa Katoliki iliyopo katika kijiji cha Kate .

“Ilikuwa Jumatatu ya Pasaka asubuhi nilikuwa nimetoka kuongoza ibada ya Misa Takatifu, basi nikashuka hadi zahanati ndipo nilipomwona mtoto huyu akiwa amelala pembeni mwa ukuta wa zahanati huku akiwa ameharibika vibaya mwilini mwake na kutoa harufu mbaya.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Martin Kazumba (36) alidai kuwa amekuwa akimpeleka mtoto wake huyo katika Kituo cha Afya kilichopo katika kijiji jirani cha Mvimwa wilayani Nkasi, kwa matibabu kwa miaka mitano mfululizo bila mafanikio.
“Tayari nimefilisika kwa ajili ya kugharamia matibabu ya mtoto wangu huyu, amekuwa akitibiwa kwa miaka mitano mfululizo bila kupona huku hali yake ikiendelea kuwa mbaya kila kukicha.
Isitoshe mke wangu, mimi mwenyewe na watoto wengine watano, akiwemo wa mwaka, tumeshaambukizwa ugonjwa huu. Nimekata tamaa sijui la kufanya hakika nimechoka inawezekana tumerogwa kwa nini ni sisi tu yaani hii familia yangu pekee ?” alihoji.
Kwa upande wake, Mganga wa Kituo cha Afya cha Kate, Abdallah alieleza kuwa ugonjwa huo kitatibu unajulikana kama Adematomycosis na kwamba mtoto huyo amepatwa na usugu wa ugonjwa huo wa ngozi, unaosababishwa na fangasi.
“Ugonjwa huu ni hatari kwa sababu unaambukiza na unaweza kuenea kirahisi katika jamii nzima na kusambaa zaidi lakini licha ya kuwa ni hatari bado unatibika. Tatizo mtoto huyu hawezi kulazwa kwa matibabu katika zahanati na vituo vya afya kwani anahitaji uangalizi maalumu. Nashauri apelekwe katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa iliyoko katika Mji wa Sumbawanga, ambako kuna wataalamu, mtoto huyu anatakiwa awe chini ya uangalizi wa jopo la wataalamu wa afya,” alisema.

No comments