Update:

01 March 2017

WHO: Wasomali zaidi ya milioni moja wanakabiliwa na hatari ya kifoShirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuhusu uzima na maisha ya zaidi ya Wasomali milioni moja wanaosumbuliwa na baa la njaa.

WHO imetahadharisha kuhusu njaa kali inayosababishwa na ukame nchini Somalia na kutangaza kuwa, maisha ya watu milioni moja na nusu yanakabiliwa na hatari kubwa.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani imesema kuwa, kwa sasa nusu ya jamii ya watu wa Somalia pekee ndio wanaoweza kupata huduma za mwanzo kabisa za afya.

Ripoti zinasema kuwa njaa iliyotokea katika baadhi ya maeneo ya Somalia mwaka 2011 ilisababisha vifo vya watu wasiopungua laki mbili na elfu 60.
Wasomali wengi wanasumbuliwa na njaa, umaskini


Baa hilo la njaa nchini Somalia linachangiwa na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na vita vya ndani, ukame na hatua za kundi la kigaidi la al Shabab ya kuzuia kupelekwa misaada ya kibinadamu katika maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji wa kundi hilo.

Ripoti iliyotolewa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa nusu ya misaada ya chakula inayotumwa Somalia inaangukia katika mikono ya mafisadi, wapiganaji wa kundi la al Shabab na magenge ya kieneo.
credit:par today