Update:

WATUHUMIWA WA MAKONTEINA BANDARINI WAPANDISHWA KIZIMBANI

Wafanyabiashara watatu akiwemo raia wa Zambia mmoja  wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma  za uhujumi uchumi ikiwemo kusafirisha bidhaa kwa kificho

Washtakiwa hao ambao wamefikishwa mbele ya Mahakimu wawili tofauti ni Sultani  Ibrahimu, (36), mwarabu Mkazi wa Usalama Temeke, Augustino Kalumba (39)  raia wa Zambia na Ramadhani Hamisi maarufu kama Ukwaju (48) anaishi
Kinondoni Hananasifu.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume na sheria ya Umoja wa nchi za Afrika Mashariki ya kudhibiti ushuru. Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba washtakiwa Sultan Ibrahimu na  Augustino Kalumba wamesomewa mashtaka matatu, la kula njama,  kusafirisha Mali iliyofichwa na kuitia hasara serikali ya Jamuhuri wa  Muungano wa Tanzania zaidi ya  shilingi milioni 287.8.
Mwendesha  mashtaka Nassoro Katuga akisaidiana na Wakili Batlida Mushi amedai kuwa  kati ya Decemba 1 mwaka jana na Machi 1 mwaka huu katika eneo
lisilojulikana washtakiwa hao wakiwa na wenzao ambao bado hawajakamatwa
walikula njama ya kusafirisha mali.
Katika shtaka la pili imedaiwa kuwa kati ya Decemba 1 hadi 31, mwaka jana katika makao makuu ya  Bandari ya Tanzania yaliyopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam  washtakiwa waliingiza magari matatu ambayo ni Range Rover sports, Zenye  naomba tofauti tofauti.
Imedaiwa kuwa magari hayo yalikuwa
yamepakiwa pamoja na nguo za mitumba na viatu kwenye kontena namba MSKU
9914168 kwa nia ya kuwadanganya maafisa wa ushuru.
Aidha  washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuingiza Mali hizo wakiwa
wamezificha na kuisababishia serikali ya Tanzania kuingia hasara zaidi
ya shilingi 287.8.  Mbele ya Hakimu Respiciou Mwijage washtakiwa Sultan Ibrahim na Ramadhani Hamis wamesomewa mashtaka matatu.
Imedaiwa kuwa kati ya Decemba Mosi mwaka jana na March 4 mwaka huu jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la Kuficha Mzigo
wakati wakiuingiza nchini.
Aidha  pamoja  na washtakiwa hao waliingiza Mzigo wa magari matatu wakiwa wameyaficha ili kuweza kuwaficha maafisa ushuru.

Wakili Katuga amedai kuwa kitendo hicho kimeikosesha serikali ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania mapato  zaidi ya shilingi milioni 190.9. Hata hivyo washtakiwa hao  hawakuruhisiwa kujibu kitu chochote na wamerudishwa rumande kwa kuwa  mashtaka dhidi yao yako chini ya sheria ya uhujumu uchumi ambayo  Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kutoa dhamana.Aidha Wakili Katuga  aliiarifu mahakama kuwa DPP bado hajatoa kibali kwa mahakama ya Kisutu  kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo itatajwa mahakamani hapo Aprili 12 mwaka huu. Upelelezi bado haujakamilika.

No comments