Update:

Rais wa Nigeria kurejea nchini leo; Baada ya matibabu UK

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria anatazamiwa kurejea nchini humo leo baada ya mapumziko yake ya matibabu nchini Uingereza yaliyoongezewa muda.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana mjini Abuja na ofisi ya rais huyo.
"Rais Muhammadu Buhari anatarajiwa kurejea nchini kesho Machi 10, 2017", imeeleza taarifa hiyo na kuongeza kuwa kiongozi huyo anathamini dua na salamu za kumtakia heri alizotumiwa na Wanigeria wa ndani na nje ya nchi.
Buhari mwenye umri wa miaka 74 aliondoka nchini Nigeria tarehe 19 Januari kuelekea Uingereza kwa safari ya matibabu. Awali alikuwa amepanga kubakia nchini humo kwa muda wa siku 10 lakini akarefusha safari yake hiyo baada ya kushauriana na madaktari wake.
Rais Buhari akiwa na Askofu Mkuu wa Canterbury, Hustin Welby, London hivi karibuni
Maafisa wa serikali ya Nigeria wamekataa kutangaza maradhi aliyonayo kiongozi huyo na hivyo kuzusha shaka na wasiwasi kuhusu afya yake katika vyombo vya habari vya nchi hiyo na mitandao ya kijamii.
Ili kuondoa wasiwasi kuhusu ombwe la uongozi katika taifa hilo kubwa kiuchumi barani Afrika, serikali ya Abuja ilikuwa imesisitiza kuwa Buhari alimkabidhi mamlaka kamili ya kukaimu urais Makamu wake Yemi Osinbajo kwa muda wote yeye akiwa mapumzikoni

No comments