Update:

16 March 2017

PROFESA JAY AFUNGUKA KUHUSU VIDEO YA WIMBO WAKE ‘KIBABE’

Baada ya kuiteka mitaa na vyombo vya habari kwa wimbo wake mpya alioubatiza jina la ‘Kibabe’, uliopata mapokezi ya kishindo cha aina yake, Profesa Jay ameweka wazi ujio wa video ya wimbo huo aliyodai pia itakuwa ya kibabe.
 Mchenguaji huyo nguli amesema kuwa tayari video ya wimbo huo imekamilika ikiwa imetayarishwa na muongozaji Hanscana.
Profesa Jay ambaye pia ni mbunge wa Mikumi amesema kuwa video hiyo imefanyika hapa nchini na imechukuliwa katika mazingira yanayovutia ikiwa ni pamoja na mbuga za wanyama za Mikumi.
“Unajua mimi ni mbunge ninayeongoza Watu na Wanyama,” Profesa aliiambia Dar24 akirejea moja ya mistari kwenye ngoma yake.
“Kwahiyo tulipata nafasi ya kushuti video nzuri sana, kuna maeneo ya mbuga ya wanyama ya Mikumi na mambo mengine ambayo ni surprise nzuri kwa watakaoishuhudia. Hii video ni burudani lakini pia ni sehemu ya kuitangaza sekta ya Utalii nchini,” Dar24 inamkariri Profesa Jay.
“Video inaweza kutoka muda wowote, kuna vitu vichache tu tunakamilisha ili mashabiki waendelee kupata kile walichokimiss kutoka kwa Profesa Jay,” alifunguka.
Mkali huyo mwenye zaidi ya miaka 25 kwenye muziki akiweka heshima inayotosha kuitwa ‘The Icon’,  amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kuitazama video kali ambayo itaaonesha kuwa hakuna ulazima wa kwenda Afrika Kusini kutafuta maeneo ya kufanyia video kwakuwa hapa nchini kuna maeneo yanayovutia na yanayowakusanya hata wageni kuja kuyatazama.
Endelea kutembelea Dar24.com uwe wa kwanza kuiangalia video ya wimbo wake, ‘Kibabe’.