Update:

Nchi tano kuunganishwa na meli mpya Kyela

Kaimu Mkuu wa Bandari ya Itungi ­ Kyela katika Ziwa Nyasa mkoani Mbeya, Ajuaye Msese amesema biashara kati ya Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Afrika Kusini na Malawi imepata huduma mpya baada ya meli mbili mpya kuanza majaribio.
Msese amesema iwapo majaribio hayo yatakamilika na meli hizo kuwa salama kwa ajili ya utoaji wa huduma, wananchi wa pande hizo wataweza kuendesha shughuli zao kwa ufasaha.

Meli mbili za mizigo zilizotengenezwa na Kampuni ya Songoro Marine zimeshushwa katika ziwa hilo kwa ajili ya majaribio baada ya kukamilika kwa asilimia 95.


Meli hizo ni kati ya tatu, ikiwamo ya abiria zinazojengwa kwa gharama ya Sh20 bilioni. Msese amesema: “Kila (meli) moja itakuwa na uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo tofauti na zilizopo zinabeba tani 720, hivyo kukamilika kwa meli hizi tutakuwa tumeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji wa majini badala ya kuendelea kusafirisha mizigo kwa barabara”.


Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Saleh Songoro amesema kitakachofuata ni matengenezo madogo na ukaguzi wa ubora kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

No comments