Update:

NAPE KUWACHONGEA VIONGOZI WANAOKALIA TAARIFA


 

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye amesema kuna athari kubwa za kutotoa taarifa muhimu na za wazi zinazohitajika na wananchi hivyo kuwanyima haki ya kujua utendaji wa Serikali.


Waziri Nape alisema kwa sasa utoaji wa habari na taarifa za Serikali kwa umma si utashi tena wa Afisa Habari au kiongozi wa Ofisi ya Umma bali ni matakwa ya kisheria ambayo yamewekewa kanuni na misingi katika Sheria za Huduma ya Habari na Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa za 2016.


“Kwa sasa kutoa habari zilizo wazi tena kwa wakati, sio utashi wa mtu tena bali ni matakwa ya Sheria hivyo ni wajibu wa kiongozi kutoa taarifa kwa umma” alisisitiza Waziri Nape.


Aidha alisema kuna baadhi ya Maafisa Mawasiliano ambao mpaka mwaka unakwisha hawajawahi kuandika taarifa yoyote kwa umma wala kutoa ufafanuzi kuhusu utendaji wa Serikali hivyo kuijengea Serikali taswira mbaya kwa Wananchi.


“Katika awamu hii hakuna “Mungu Mtu” katika utoaji wa taarifa hivyo ni wajibu wa viongozi kutoa taarifa au ufafanuzi pale inapohitajika na sio kukwepa waandishi wa habari, na kutofuatilia kero za Wananchi ” alisema Waziri Nape.


Waziri Nape aliwataka Maafisa Mawasiliano na Viongozi katika Taasisi za umma nchini kutekeleza Sheria ipasavyo kwa kutoa habari na taarifa kwa umma bila urasimu.


“Ndugu zangu msikalie taarifa maana kama hutoi ushirikiano kwa wana habari na wote wanaohitaji taarifa watatunga zakwao ,hapo sasa mnaanza kukimbizana kukanusha” ,Alisisitiza Waziri Nape.