Update:

02 March 2017

Kanisa katoliki lajiunga na watetezi wa haki za binadamu, laitaka serikali kukomesha mauaji dhidi ya raia CongoKanisa Katoliki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limetahadharisha kuhusu utendaji wa jeshi la serikali ya nchi hiyo katika mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa kundi la Kamounia Nsap kwenye mkoa wa Kasai.

Tahadhari hiyo ya Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokraia ya Congo imetolewa baada ya jumuiya za kikanda na kimataifa kukemea mauaji ya raia yanayofanywa na jeshi la Congo DR katika mikoa ya Kasai, Kasai Kati, Kasasi Oriental na Lomami. Taarifa ya kanisa hilo imesema mauaji hayo ni maafa makubwa na limetoa wito wa kukomeshwa ukatili katika mkoa wa Kasai.

Askofu FĂ©licien Mwanama pia amewataka wanamgambo wa kundi la Kamounia Nsap kukomesha uhasama na jeshi la serikali ya Congo na ameishauri serikali ya Kinshasa kuwa na uvumilivu.
Jeshi la Congo DR linatuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia

Yapata siku kumi zilizopita Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein alisema serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina wajibu wa kuchunguza ripoti za kuaminika kuhusu jinai zilizofanywa nchini humo yakiwemo mauaji ya raia yaliyofanywa na jeshi.

Taarifa ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa wakati umefika wa kukomesha utumiaji nguvu butu za kijeshi ambazo hazina taathira yoyote katika kushughulikia chanzo cha mgogoro kati ya serikali na wanamgambo na badala yake kuwalenga raia kwa msingi wa madai ya kuwa na mafungamano na wanamgambo hao.