Update:

Felix Tshsekedi arithi mikoba ya baba yake Kongo DR

Chama kikuu cha upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimemteua Felix Tshisekedi kuwa kinara wa chama hicho kufuatia kifo cha baba yake, Etienne Tshisekedi.
Jose Endundo, mmoja wa viongozi wa chama cha upinzani cha UDPS ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, Felix Tshisekedi ameteuliwa kuwa mkuu wa chama hicho ingawaje majukwaa mawili kati ya tisa ya chama hicho yamepinga uteuzi huo.
Aidha UDPS imemteua Pierre Lumbi, mfuasi wa zamani wa Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kuwa mkuu wa tawi la masuala ya siasa la chama hicho cha upinzani, akimbwaga Martin Fayulu ambaye amelalamikia mchakato wa uteuzi huo. Ameonya kuwa huenda uteuzi huo ukazusha mpasuko mkubwa ndani ya upinzani.
Marehemu Etienne Tshisekedi
Mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Februari, kiongozi mkongwe wa upinzani Kongo DR, Mzee Etienne Tshisekedi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84 nchini Ubelgiji. Tshisekedi alielekea mjini Brussels nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu ya kiafya mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
Tshisekedi aliaga dunia katika hali ambayo, chama chake kinaendelea na mazungumzo ya kugawana mamlaka kufuatia hatua ya Rais Joseph Kabila kukataa kujiuzulu baada ya muda wake wa uongozi kumalizika mwaka uliopita.

No comments