Update:

DC ashangazwa na ujasiri wa wakulima wa bangi

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, Godfrey Ngupula ameshangazwa na ujasiri walionao wananchi wanaolima mashamba makubwa ya bangi licha ya jitihada za Serikali kuzuia zao hilo haramu.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwa kwenye operesheni ya kukamata na kuteketeza bangi, Ngupula alisema baadhi ya wananchi wamegeuza hifadhi ya Igombe iliyopo mpakani mwa wilaya za Nzega na Uyui mkoani humo imegeuzwa kuwa mashamba ya bangi.
“Sijawahi kuona watu wanalima bangi kwa kujiamini kiasi hiki tena kwa wingi kama hakuna Serikali, tutahakikisha bangi yote inateketezwa na watuhumiwa wote kufikishwa mahakamani,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Alitoa wito kwa jamii katika maeneo hayo kuacha kilimo hicho haramu na kuondoka kwa hiari katika hifadhi kabla operesheni maalumu haijaanza ya kupambana na wahalifu misitu. Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mambali jirani na hifadhi hiyo waliiomba Serikali kuendelea na operesheni ili kukomesha biashara na kilimo cha bangi kinachosababisha uhalifu kuongezeka.
source: mwananchi

No comments