Update:

03 February 2017

Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu ukame unaoikabili SomaliaUmoja wa Mataifa umetangaza kuwa nchi ya Somalia inakabiliwa na ukame na hivyo kuiongezea matatizo nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayokabiliwa pia na tatizo la njaa na ukosefu wa amani na usalama.

Peter de Clercq, Mratibu wa Umoja wa Mataifa Katika Masuala ya Kibinadamu nchini Somalia amewaambia waandishi wa habari mjini Mogadishu kwamba, endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo, katika kipindi cha miezi sita ijayo, Somalia itakabiliwa na maafa na ukame mkubwa ambao madhara yake hayawezi kutasawarika.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa Katika Masuala ya Kibinadamu nchini Somalia amesema kuwa, kwa kuzingatia uhaba wa chakula unaoikabili nchi hiyo kwa sasa, wananchi wengi wanahitajia misaada ya haraka ya chakula.
Wanyama wanakufa kwa kukosa malisho katika baadhi ya nchi za Afrika

Siku chache zilizopita pia, Peter de Clercq alinukuliwa akitangaza kuwa, hali ya kibinadamu kwa mamilioni ya wananchi wa nchi hiyo inatia wasiwasi ikiwa ni natija ya kushadidi ukame nchini humo.

Aidha alisema kuwa, takribani watoto laki tatu na elfu ishirini wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe duni na kwamba 50 elfu kati yao wana hatari ya kupoteza maisha endapo hawatapatiwa msaada wa haraka. Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, nusu ya wananchi wa Somalia hawana uwezo kamili wa kupata chakula.

Mbali na majanga hayo ya kimaumbile, Somalia inakabiliwa pia na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo limekuwa likifanya mashambulizi ya kigaidi nchini humo.