Update:

28 February 2017

Rais Barrow amfuta kazi mkuu wa jeshi Gambia na makanda 10Rais Adama Barrow wa Gambia amempiga kalamu nyekundu Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo, Jenerali Ousman Badjie, pamoja na makamanda wengine 10 wa ngazi za juu wa vikosi vya usalama nchini humo.

Msemaji wa Jeshi, Kanali Kemo Kanuteh amesema nafasi ya Jenerali Badjie imejazwa na Masanneh Kinteh, ambaye amekuwa mshauri wa Rais Barrow katika masuala ya kijeshi tokea Januari mwaka huu.

Duru za kijeshi zimearifu kuwa, mbali na Jenerali Badjie, makanda wengine 10 wa jeshi la nchi hiyo wamefutwa kazi, wakiwemo wakurugenzi wa operesheni na intelijensia waliofanya kazi chini ya utawala wa rais wa zamani Yahya Jammeh.

Huku hayo yakiarifiwa, David Colley, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Magereza aliyepigwa kalamu nyekundu hivi karibuni yuko kizuizini baada ya kutiwa mbaroni na polisi jana Jumamtatu.

Rais wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh aliyeongoza kwa miaka 22

Wiki iliyopita, Rais Barrow aliamuru kutiwa mbaroni kamanda wa zamani wa idara ya usalama wa taifa ya Gambia, Yankuba Badjie. Kamanda huyo aliyeongoza idara ya usalama wa taifa ya Gambia katika kipindi cha rais wa zamani wa nchi hiyo Yahya Jammeh, aliogopwa sana kote nchini.

Siku chache zilizopita, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilitoa ripoti iliyoeleza kwamba, serikali ya Jammeh ilikuwa ikitumia vitisho na utesaji dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani na wakosoaji sambamba na kuwanyima haki zao za msingi.