Update:

19 January 2017

Tahadhari Afrika Mashariki baada ya Homa ya ndege kuibuka Uganda

Nchi za Afrika Mashariki zimeanza kuchukua tahadhari siku chache baada ya mlipuko wa homa ya mafua ya ndege (Avian Flu) kugunduliwa nchini Uganda.
Serikali ya Tanzania inajiandaa kuunda timu ya wataalamu kutathmini hali ya ugonjwa huo katika Kanda ya Ziwa. Rwanda pia imetangaza hali ya tahadhari, na sasa wizara ya afya ya nchi hiyo inashirikiana na mashirika husika kuangalia kwa karibu hali ya ugonjwa huo na kuchukua hatua kuuzuia usiingie Rwanda.
Nchini Kenya Waziri wa Kilimo Willy Bett Jumatano alipiga marufuku uagizaji ndege na mazao yao, mfano mayai, kutoka Uganda kwa kuhofia maambukizi ya maradhi ya mafua ya ndege. Aidha alisema wamewasiliana na maafisa wa mifugo nchini Uganda ili wasitoe vibali vyovyote vya kusafirisha ndege na mazao yao kuingia Kenya. “Vibali vya uagizaji ndege au mazao yao vilivyotolewa kabla ya tangazo hili pia vimepigwa marufuku vyote,” alisisitiza Bw Bett.
Shamba la Kuku
Vilevile, juhudi za kufuatilia maambukizi hayo zimepigwa jeki huku maeneo kunapotua ndege wa porini hasa kunywa maji, sehemu za kuuza ndege walio hai na vichinjio vikimulikwa kwa makini.
Nchi tatu za Afrika mashariki Tanzania, Kenya na Rwanda zote zimetangaza marufuku ya kuagiza ndege kutoka Uganda na nchi nyingine za Ulaya zinazowezekana kukumbwa na ugonjwa huo.