Update:

16 January 2017

Serikali ya Russia yaafikiana na Trump kuhusu NATO

Ikulu ya Russia (Kremlin) imetangaza kuwa serikali ya nchi hiyo inaafiki mtazamo wa Rais Mteule wa Marekani Donald Trump kwamba Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) umepitwa na wakati.
Dmitry Peskov msemaji wa Ikulu ya Kremlin amesema kuwa muungano wa Nato ni ukumbusho wa zama zilizopita ambao ulikuwa ukijielekeza katika mapambano na makabiliano na pande nyingine. Amesema muundo mzima wa muungano huo pia umebadili taswira ya makabiliano ya muungano huo. Peskov ameongeza kuwa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi umeweza kwa tabu kutajwa kama mfumo wa kisasa wenye uwezo wa kudhamini amani, uthabiti na ustawi wa kudumu na usalama.

Vikosi vya Muungano wa Nato 
Kabla ya matamshi haya ya msemaji wa Ikulu ya Russia, Donald Trump Rais mteule wa Marekani alisema katika mahojiano na gazeti la Times la Uingereza na lile la Bild la Ujerumani kwamba, Muungano wa Nato umepitwa na wakati kwa kuwa umeshindwa kukabiliana na ugaidi. Trump alisema kuwa nchi wanachama wa Nato hazitekelezi majukumu yao; kitendo ambacho si cha uadilifu.