Update:

20 January 2017

Rais Yahya Jammeh wa Gambia akubali kukabidhi madaraka

Baada ya kutokea mivutano mikubwa ya kisiasa, hatimaye Rais Yahya Jammeh wa Gambia amekubali kuondoka madarakani.
Mwandishi wa Radio Tehran amezinukuu duru mbalimbali za barani Afrika zikisema kuwa, Rais Yahya Jammeh amekubali kukabidhi madaraka kwa masharti maalumu.
Hatua hiyo imekuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura ya kumtaka aondoke madarakani na akabidhi madaraka kwa rais aliyechaguliwa na wananchi.
Kabla ya hapo Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS ililitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati suala la Gambia na kutoruhusu Rais Yahya Jammeh akanyage demokrasia.
Adama Barrow akila kiapo cha kuwa Rais wa Gambia katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Dakar Senegal, Alkhamisi, Januari 19, 2017

Huku hayo yakiripotiwa, wanajeshi wa nchi jirani ya Senegal wameripotiwa kuingia katika ardhi ya Gambia kwa ajili ya kumuunga mkono Adama Barrow ambaye jana aliapishwa kuwa Rais wa Gambia akiwa katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Dakar, Senegal.
Ecowas mara kadhaa ilimtaka Rais Yahya Jammeh wa Gambia akabidhi madaraka kwa amani baada ya kuitawala nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kwa muda wa miaka 22.
Jammeh alishindwa kwenye uchaguzi uliofanyika tarehe Mosi Disemba mwaka jana na awali alitangaza hadharani kukubali kushindwa, lakini baadaye alibadilisha msimamo na kudai kuwa kumefanyika udangayifu mkubwa kwenye uchaguzi huo.