Update:

27 January 2017

Rais wa GAMBIA apokelewa kwa furaha na wananchiWananchi wa GAMBIA walikuwa na furaha wakati walipomkaribisha nyumbani RAIS ADAMA BARROW, ambaye alichaguliwa miezi miwili iliyopita lakini akalazimika kukimbilia nchini SENEGAL baada ya mtangulizi wake kukataa kuachia madaraka.

Akiwa amevalia kanzu nyeupe na kofia, BARROW alishuka kwenye ndege siku ya Alhamisi, akiwa amezingiriwa na vikosi vya wanajeshi kutoka nchi za SENEGAL na NIGERIA baada ya kuwasili nchini mwake akitokea SENEGAL ambapo alipewa hifadhi tangu JANUARI 15.

Ujio wake ni ishara kwa GAMBIA kuhamisha madaraka kwa mara ya kwanza kwa njia ya kidemokrasia katika nchi hiyo ndogo ambayo ilikuwa koloni la Uingereza baada ya kiongozi wa muda mrefu YAHYA JAMMEH kukataa kuachia ofisi baada ya kushindwa katika uchaguzi DESEMBA 1 mwaka uliopita.

BARROW alikula kiapo cha uongozi akiwa katika ubalozi wa nchi yake mjini DAKAR wiki iliyopita huku vikosi vya mataifa mbalimbali barani AFRIKA vikiingia nchini GAMBIA kumhakikisha usalama wake na kuondoka kwa JAMMEH.