Update:

18 January 2017

Raia mia moja wauawa katika shambulizi la Jeshi la Anga la Nigeria

Makumi ya watu wameuawa katika shambulizi lililofanywa na ndege za kivita za Nigeria dhidi ya kambi moja ya wakimbizi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka imetangaza kuwa, watu wasiopungua 100 wameuawa na wengine 120 kujeruhiwa katika shambulizi hilo la Jeshi la Anga la Nigeria katika eneo lililoko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Cameroon.
Kamanda wa jeshi la Nigeria Meja Jeneral Lucky Irabor amethibitisha kuwa shambulizi hilo lililotekelezwa katika eneo la Rann limelenga kwa makosa kambi ya wakimbizi lakini amekataa kutoa takwimu kamili kuhusu idadi ya raia waliouawa katika shambulizi hilo.
 
Wakati huo huo Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetangaza kuwa wafanyakazi wake 6 ni miongoni mwa waliouawa katika shambulizi hilo lililofanyika katika jimbo la Borno. Wafanyakazi wengine kadhaa wa shirika hilo na lile la Madaktari Wasio na Mipaka pia wamejeruhiwa.
Shambulizi hilo lilifanyika kwa shabaha ya kulenga wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram lakini likapiga kwa makosa kambi ya wakimbizi katika eneo la Rann.