Update:

17 January 2017

Mtoto wa Rais mteule wa Gambia afariki kwa kushambuliwa na mbwa

Mtoto wa kiume wa Rais-mteule wa Gambia mwenye umri wa miaka minane amefariki dunia kwa kushambuliwa na mbwa katika mazingira ya kutatanisha, wakati huu ambapo baba yake yuko nchini Senegal.
Familia ya Rais-mteule wa Gambia imesema Habibou Barrow alizikwa jana nyakati za adhuhuri katika makaburi ya Kanifing, kwenye viunga vya mji mkuu Banjul. Baadhi ya watu wa familia ya Adama Barrow wamenukuliwa na vyombo vya habari wakisema kuwa mwana wa kuiume wa rais huyo mteule ambaye yuko Senegal hivi sasa alifariki dunia baada ya kushambuliwa na mbwa Jumapili jioni.
Hata hivyo maelezo zaidi kuhusiana na kifo cha Habibou Barrow, ambaye ni kati ya watoto watano wa Rais-mteule wa Gambia hayajatolewa na familia wala Adama Barrow mwenyewe. 
Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow

Hivi karibuni msemaji wa Barrow alisema sherehe ya kumuapisha mfanyabiashara huyo zitaendelea kama zilivyopangwa Alkhamisi ijayo jijini Bunjul. 
Hatua ya Barrow kwenda Senegal ilichukuliwa na viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS walipokutana nchini Mali mwishoni mwa wiki. Hii ni baada ya Rais Yahya Jammeh kuendelea kung'ang'ania madaraka akisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho wa kadhia hiyo utatolewa na mahakama.
Jammeh ambaye ameiongoza Gambia kwa miaka 22 alishindwa kwenye uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe Mosi mwezi uliopita wa Disemba na awali alikubali kushindwa, lakini baadaye alibadilisha msimamo na kudai kuwa kumefanyika udanganyifu katika kuhesabu kura.
Rais Yahya Jammeh wa Gambia