Update:

17 January 2017

Mbeya: Maiti iliyozikwa yakutwa chumbani kwenye godoro.

  Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio mbalimbali huku kukiwa na na tukio moja la taarifa ya kifo kama ifuatavyo Mnamo tarehe 16.01.2017 majira ya saa 10:30 Asubuhi huko Igoma “A”, Kata ya Isanga, Tarafa ya Sisimba, Jeshi llilipokea taarifa kuwa maiti iliyokwenda kuzikwa katika makaburini ya zamani ya Isanga kukutwa nyumbani, chumbani ikiwa kwenye godoro.

Kwa mujibu wa taharifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Emmanuel G. Lukula imesema kuwa mara baada ya Polisi kupata taharifa walifuatilia na kubaini kuwa tarehe 16.01.2017 majira ya saa 07:00 Asubuhi Mtu mmoja aitwaye Jailo Kyando[36] Muosha magari na mke wake aitwaye Anna Elieza [32] wote wakazi wa Mtaa wa Igoma “A” waliamka asubuhi na kukuta mtoto wao wa kwanza aitwaye Harun.J. Kyando [09] amefariki dunia akiwa amelala.

“Taarifa za awali zinadai kuwa marehemu tangu utoto wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa kifafa hali iliyopelekea kuishi nyumbani pasipo kusoma. Kufuatia kifo hicho msiba uliendeshwa na taratibu za mazishi zilifanyika. Majira ya saa 12:00 Mchana jeneza lililoletwa msibani na kuwekwa sebuleni kando ya mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeviringishwa na blanketi na kulazwa chini kwenye godoro, baada ya maombi yaliyoongozwa na walokole waitwao Bonde la Baraka vijana walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani ya Isanga na kisha jeneza kuzikwa. Amesema Kamanda .
 
Amesema kuwa Waombolezaji waliporudi nyumbani walitaharuki kuona mwili wa marehemu Mtoto Harun.J. Kyando ukiwa chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali. Kutokana na hali hiyo taarifa zilifikishwa Polisi mara moja, askari Polisi walifika na kurejesha hali ya amani kwa kuuchukua mwili wa marehemu ambao kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Amesema kuwa Taratibu nyingine za mazishi zitafanyika leo tarehe 17.01.2017. Mpaka sasa bado haijafahamika ni uzembe /bahati mbaya wafiwa kusahau kuweka mwili wa marehemu kwenye jeneza au kulikuwa na hujuma zozote. Upelelezi unaendelea kuhusiana na tukio hili.


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Emmanuel .G. Lukula anatoa wito kwa jamii kuacha kutumia dawa za kulevya na Pombe Moshi [Gongo] kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya ya mtumiaji.


Aidha Kamanda Lukula anatoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri za uhalifu na wahalifu ili kupunguza matukio ya uhalifu na wahalifu katika mkoa wetu.