Update:

17 January 2017

Iran yajibu barua ya Saudi Arabia kuhusu mwaliko wa Hija

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejibu mwaliko rasmi uliotumwa na Saudi Arabia kuhusu kushiriki katika mikutano ya kujadili sual la kushiriki tena Wairani katika ibada ya Hija mwaka huu.
Hujjatul Islam wal Muslimin Sayyid Ali Qadhi-Askar, mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei katika masuala ya Hija na Ziara, amesema kuwa Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran, Ridha Salehi-Amiri, amejibu mwaliko wa Saudia kupitia barua aliyomwandikia Waziri wa Hija wa Saudia Mohammed Bentin.
Jumatatu wiki hii Qadhi- Askar alithibitisha kuwa, Iran imepokea rasmi mwaliko wa Saudia kushiriki katika vikao vya Hija. Aidha amebainisha matumaini yake kuwa mazungumzo hayo yatakuwa na natija nzuri ili kuwezesha ibada ya kimaanawi ya Hija ifanyike mwaka huu.
Maafa ya Mina katika Ibada ya Hija Septemba, 2015
Mnamo Septemba 2015, kulijiri msongamano mkubwa wakati wa ibada ya Hija katika eneo la Mina karibu na Makka ambapo duru zisizo rasmi zinasema Mahujaji 7,000 walipoteza maisha huku Saudia ikisisitiza ni watu 770 waliouawa katika msongamano huo. Iran ilitangaza kuwa mahujaji wake wapatao 465 walipoteza maisha katika maafa hayo ya Mina. Siku kadhaa kabla ya tukio hilo, Mahujaji 100 walipoteza maisha katika Msikiti Mtakatifu wa Makka, wakiwemo Wairani 11 baada ya winchi kuwaangukia wakati wanapotufu.
Maswali mwengi waliibuka kuhusu uwezo wa Saudi Arabia kusimamia zoezi la Hija ambapo mwaka jana Iran ilitaka usalama wa Mahujaji wake udhaminiwe. Kufuatia sisitizo hilo la Iran, Saudi Arabia iliwazuia mahujaji Wairani kushiriki katika ibada ya Hija.