Update:

19 January 2017

Bunge la Nigeria kuchunguza hujuma ya ndege za kivita dhidi ya kambi ya wakimbizi

Bunge la Nigeria limesema litachunguza shambulizi la anga lililofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya kambi ya wakimbizi kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno
Kwa mujibu wa gazeti la Nigeria Today, bunge litachunguza hujuma hiyo ili kuthibitisha kama shambulizi hilo lilifuata Sheria ya Anga na Kibinadamu ya Kimataifa au la. Watu zaidi ya 52 waliuawa na wengine 120 kujeruhiwa kwenye shambulizi hilo, ambalo jeshi limelitaja kuwa ni dosari ya kiutendaji.
Hata hivyo Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka imetangaza kuwa, ni watu wasiopungua 100 ndio waliouawa na wengine 120 kujeruhiwa katika shambulizi hilo la Jumanne la Jeshi la Anga la Nigeria katika eneo lililoko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Cameroon.


Kamanda wa jeshi la Nigeria Meja Jeneral Lucky Irabor amethibitisha kuwa shambulizi hilo lililotekelezwa katika eneo la Rann lililenga kwa makosa kambi ya wakimbizi lakini amekataa kutoa idadi kamili ya raia waliouawa katika shambulizi hilo. 
Shambulizi hilo lilifanyika kwa shabaha ya kulenga wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram lakini likapiga kwa makosa kambi ya wakimbizi katika eneo la Rann.
Credit :Pars Today