Update:

19 January 2017

Baraza la Usalama laitisha mkutano wa dharura kuhusu Gambia, taharuki yatanda nchini humo

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya mkutano wa dharura hii leo kuhusiana na mgogoro wa kisiasa na kunukia machafuko ya umwagikaji damu nchini Gambia.
Duru za kidiplomasia zimearifu kuwa, nchi wanachama wa Baraza la Usalama zinakutana leo Alkhamisi kupigia kura azimio lililoandaliwa na nchi za magharibi mwa Afrika, la kutaka Rais Yahya Jammeh wa Gambia ashinikizwe kukabidhi madaraka kwa Rais mteule Adama Barrow ambaye kwa sasa yuko nchini Senegal.
Wakati huo huo, viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS wanafanya mkutano wa dharura nchini Senegal hii leo kujadili mustakabali wa Gambia.
Huku yako yakiarifiwa, Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Gambia, Ousman Badjie amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo ndogo ya magharibi ya Afrika hawatakabiliana na askari wa kieneo watakaotumwa nchini. Amesema: "Huu ni mgogoro wa kisiasa, sisi kama jeshi hatutajiingiza kwenye mzozo huu, iwapo vikosi vya kieneo vitaingia nchini, nitawaagiza wanajeshi wangu kusalimu amri kwa kunyanyua mikono juu."
Vikosi vya eneo la magharibi mwa Afrika vyatumwa mpakani mwa Gambia
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Anga la Nigeria imesema kuwa, kundi la askari 200, ndege kadhaa za kivita, manwari ya kijeshi, helikopta na ndege za ujasusi zimepelekwa nchini Senegal kwa ajili ya kufuatilia hali ya mambo nchini Gambia. 
Hatua hiyo imechukuliwa huku nchi za Magharibi mwa Afrika zikijitayarisha kutuma majeshi nchini Gambia kwa ajili ya kumuondoa madarakani kwa nguvu Jammeh ambaye kipindi chake cha uongozi kinamalizika leo.
Adama Barrow, Rais mteule wa Gambia
Hii ni katika hali ambayo, vyombo vya habari nchini Senegal vimeripoti kuwa hakuna dalili wala harakati zozote za kufanyika sherehe za kumuapisha Rais mteule wa Gambia Adama Barrow nchini humo.
Hapo jana Halifa Sallah, msemaji wa Adama Barrow alisema kuwa, ikibidi, Rais huyo mteule wa Gambia ataapishwa leo katika ubalozi wa Gambia nchini Senegal.  
Rais Yahya Jammeh anayeng'ang'ania madaraka nchini Senegal
Hapo jana Bunge la Taifa la Gambia lilipasisha azimio la kumruhusu Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo asalie madarakani kwa miezi mitatu zaidi, siku moja baada ya Jammeh ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 22 kutangaza hali ya hatari.