Update:

18 January 2017

António Guterres: Sudan Kusini ishinikizwe kuwakubali askari wa kusimamia amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametilia shaka suala la kutumwa askari zaidi wa umoja huo nchini Sudan Kusini akisema kuwa, serikali ya nchi hiyo hairidhii suala hilo.
António Guterres ameyasema hayo katika ripoti ya siri aliyoituma kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akikosoa kitendo cha serikali ya Juba cha kutotoa ushirikiano kwa ajili ya kutumwa maelfu ya askari wa kusimamia amani nchini humo. Katika ripoti hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kuishinikiza Sudan Kusini ili ikubaliane na suala hilo.
Askari wa kofia za buluu wa Umoja wa Mataifa
Baada ya mapigano ya mwezi Julai mwaka jana mjini Juba, mji mkuu wa nchi hiyo, mwezi Agosti Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutumwa askari wengine 4,000 wa kulinda amani nchini humo. Kadhalika baraza hilo lilitishia kuwa, kama serikali ya Juba haingetoa ushirikiano katika suala hilo au kuweka vizuizi vyovyote vile, basi ingekabiliwa na vikwazo vya silaha kutoka Umoja wa Mataifa.
Mahasimu wa kisiasa nchini Sudan Kusini
Vita na machafuko nchini Sudan Kusini, viliibuka mwaka 2013, baada ya kujiri ushindani wa kimadaraka baina ya Rais Salva Kiir Mayardit na hasimu wake, Riek Machar, makamu wake wa zamani.