Update:

18 January 2017

AFCON 2017- Cameroon yaikwaruza Guinea Bissau

Mabingwa mara nne Cameroon wamekwenda kileleni katika kundi A baada ya kupigana na kupata ushindi dhidi ya Guinea Bissau wanaocheza Kombe la Mataifa kwa mara ya kwanza.
Guinea Bissau walioshangaza wengi kwa kufuzu katika michuano hii, waliongoza kupitia bao maridadi la Piquito.
Cameroon walisawazisha baada ya mapumziko kufuatia mkwaju mkali wa chini nje tu ya eneo la hatari.
Michael Ngadeu-Ngadjui alitandika shuti jingine kali na kuandikisha ushindi wa kwanza kwa Cameroon katika michuano hii tangu mwaka 2010.
Simba wa Cameroon, ambao wakati fulani walikuwa wakitawala soka la Afrika, walishindwa kufuzu katika michuano miwili kati ya mitatu iliyopita, na walipoteza mechi zao zote tatu mwaka 2015.
Hata hivyo, baada ya kutoka sare katika mchezo wa kwanza dhidi ya Burkina Faso, sasa wana nafasi kubwa ya kuingia robo fainali.
Cameroon wanaongoza kundi lao baada ya mechi nyingine kumalizika kwa sare ya 1-1.
Awali wenyeji Gabon walipigana kufa na kupona na kuokoa pointi moja baada ya kulazimisha sare dhidi ya Burkina Faso, Pierre Emerick Aubameyang akitikisa nyavu kwa upande wa Gabon.
Cameroon wanatakutana na Gabon, huku Guinea Bissau wakicheza na Burkina Faso katika mechi za siku ya Jumatatu zitakazoamua nani anasonga mbele.
Guinea Bissau lazima washinde mechi yao hiyo, iwapo wanataka kusonga mbele.