Update:

16 December 2016

SIMBACHAWENE AFAFANUA AGIZO LA RAIS MAGUFULI KUHUSU 'WAMACHINGA


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene  akitoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu agizo alilolitoa Rais Dkt John Magufuli  hivi karibuni juu ya kusitisha zoezi la kuwahamisha Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu Wamachinga, kulia kwake ni Mkurugenzi Idara ya Tawala za Mikoa TAMISEMI Susan Chekani na kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya) Dk. Zainab Chaula.

Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa wameagizwa kuhakikisha wanatekeleza agizo la Rais Dk.John Magufuli la kuwatafutia maeneo ya kufanyia biashara Wafanyabiashara ndogo ndogo ‘wamachinga’ na si kuwaacha wafanye biashara zao kiholela.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Simbachawene alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Amewataka wakuu hao kuwawekea Wamachinga utaratibu wa kupangiwa maeneo ya shughuli zao yenye wateja wa kutosha, miundombinu rafiki na washirikishwe katika michakato yote wakati wa maandalizi ya maeneo hayo.

Amefafanua kuwa Rais Magufuli alisitisha zoezi la kuwaondoa kiholela wamachinga kutoka katika maeneo wanayofanyia biashara zao kwasasa hadi pale mamlaka husika zitakapoandaa maeneo maalum kwa ajili yao.

“Maagizo ya Rais yameonesha namna anavyowapenda na kuwathamini wamachinga na aliweka msisitizo wasiondolewe mpaka pale yatakapotengwa maeneo mbadala,”amesema Simbachawene.

Amebainisha utaratibu wowote wa kuwapangia maeneo mapya uzingatie ushirikishwaji ili kuondoa msuguano wakati wa kuwahamisha na kwamba pale inapowezekana wapangiwe maeneo ya katikati ya mji ikibidi kuteua mitaa mahsusi kwa utaratibu utakaowekwa ili wafanye biashara zao.

Pamoja na maelezo hayo, Simbachawene amesema Rais alisisitiza kwamba maagizo yake juu ya wamachinga hayana maana kuwa kwasasa wamachinga wafanye biashara zao kwenye barabara za kupita magari na watembea kwa miguu au kwenye hifadhi za barabara.

Amewasisitiza wakuu hao kujipanga kutekeleza maagizo ya rais kwa ufasaha, weledi na umakini mkubwa ili kuwasaidia wamachinga kufanya biashara zao na kujipatia kipato na kuzitaka mamlaka za serikali kuheshimu shughuli zao.

Wakati huo huo, Simbachawene amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa ya Rukwa na Arusha watafute shule ndani ya mikoa yao na kuwapanga wanafunzi ambao wameondolewa shule za sekondari Makuyuni na Milundikwa ambazo majengo yake yamerudishwa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).

Amesema serikali imelazimika kuwaondoa wanafunzi 254 wa shule ya Makuyuni wa kidato cha kwanza hadi cha tatu na katika shule ya Milundikwa wanafunzi 120 wa kidato cha tano na sita.

Pia amesema walimu na watumishi wasio walimu ambao walikuwa wakifundisha katika shule hizo wapangiwe kwenye shule watakazopelekwa wanafunzi hao.

Ametaka utekelezaji huo wa agizo hilo ufanyike kabla shule hazijafunguliwa januari 2017 na lizingatie kutowavuruga wanafunzi wa kidato cha sita ambao tayari wamesajiliwa kufanya mtihani wa Taifa mwezi mei, 2017.