Update:

20 October 2016

Lema afunguka ‘bifu’ na Gambo

Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema amesema chanzo cha ugomvi kati yake na mkuu wa mkoa wa Arusha ,Mrisho Gambo ni ”Kiongozi huyo wa serikali kupenda kuingilia majukumu ya  wenzake bila sababu”
Wawili hao walipishana kauli na kusababisha vurugu wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto jijini hapa juzi.
Akizungumza na Nipashe jana kwenye eneo la Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Lema alidai Gambo ana tatizo kutokana na kula kiapo cha utii na kupewa maelekezo kuwa akifika Arusha kila kitu awe nacho kwa kuwa jiji hilo lina upinzani.
Lema alidai hakubaliani pia na uteuzi wa Gambo kutokana na Mkuu wa Mkoa huyo “kushtakiwa katika kesi tatu akiwa Mkuu wa Wilaya Korogwe na zote alishindwa”.
Kuhusu mariadhiano hasa kutokana na wote wawili kuwa viongozi wanaopaswa kuwaletea maendeleo wananchi wa Arusha kwa ujumla na jimbo la Arusha mjini? “Ikitokea viongozi wakaja Arusha kututaka tufanye maridhiano, mimi neno langu moja tu kuwa kila mtu aheshimu mipaka yake ya kazi,” alisema Lema.
Aliendelea kudai kuwa kiongozi huyo wa serikali tangu atue Arusha, amekuwa akivuruga kila mahali na kutaka kila mtu amfahamu kuwa yeye ni Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, jambo ambalo alisema si busara.
Akitolea mfano, Lema alisema walivutana mbele ya wafadhili wa mradi wa hospitali ya mama na motto (Martenity Afrika) kwa sababu Gambo alipoalikwa kama mgeni rasmi, alianza kuvuruga ratiba na kumkataza Lema kuongea chochote.
“Sasa mimi nasema siwezi kuvumilia, kama noma (na) iwe noma na sasa akileta noma hata hadharani au chumbani atajibiwa hapo hapo, kwani sisi Chadema tulitulia lakini anatuchokoza,” alisema.
Lema alisema Gambo amekuwa kiongozi ambaye kila anakokwenda anafanya siasa hata sehemu ambayo haitakiwi.
Alisema kwa mfano eneo lililowafarakanisha juzi, Gambo hafahamu historia yake lakini alianza kupiga propaganda mbele ya wafadhili. Lema anadai yeye ndiye aliywetafuta eneo hilo wakati Mkuu wa Mkoa alisema lilitolewa na mfadhili.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema anamshangaa Gambo kwa kuwa kila wanachofanya Chadema anakiponda, huku akimsifia aliyemteua.
“Kuna safari moja alipokuja Rais kuzindua jengo la NSSF na PPF mimi hawakuniweka kuzungumza chochote katika ratiba, lakini Rais akasema ‘natambua mji una wenyewe hebu Meya aseme neno’, hizo ndizo siasa za kistaarabu na tulizozoea siyo za Gambo,” alisema.
Alisema haiwezekani bosi wake akawasifia lakini yeye anakejeli kila kitu na hata alichovuruga juzi juu ya mradi huo wa hospitali ya mama na mtoto ni mradi mkubwa wa Sh. biloni tisa ambao makao makuu yake yatakuwa Arusha kwa Afrika nzima.
“Sasa angetumia busara, amekuwa mgeni rasmi angezungumza baada ya wenzake kuzungumza na kumaliza salama, lakini yeye anaanza kuamrisha kata jina la Lema, kata hili sitaki, sasa tunaleta siasa sehemu isiyotakiwa siasa, hili suala halifai na likemewe isije ikarudisha Arusha ya miaka ya nyuma ya vurugu,” alisema.
Jitihada za kumpata Gambo kwa mazungumzo ya ana kwa ana au simu zilishindana jana.
Gambo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Agosti 18, mwaka huu, akichukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Felix Ntibenda ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
By IPP MEDIA