Update:

21 October 2016

Kongamano la kimataifa kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi kwenye mtandao lafanyika Beijing

Kongamano la pili la kimataifa kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi kwenye mtandao, lililoandaliwa na Baraza la kimataifa la mapambano dhidi ya ugaidi, limefanyika leo hapa Beijing. Watu wapatao 180 wakiwemo wajumbe kutoka nchi wanachama wa baraza hilo, maofisa wa mashirika ya kimataifa, wataalamu na wawakilishi wa makampuni ya huduma za mtandao wa internet, wamehudhuria kongamano hilo.
Mwaka 2014, China ilifanikiwa kuandaa kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi kwenye mtandao chini ya utaratibu wa Baraza la kimataifa la mapambano dhidi ya ugaidi. Mkutano wa mwaka huu ni hatua nyingine muhimu inayochukuliwa na jumuiya ya kimataifa katika hali mpya ya vita dhidi ya ugaidi, chini ya kaulimbiu ya "kukusanya maoni ya pamoja, kupanua ushirikiano na kupambana kwa ufanisi na ugaidi kwenye mtandao."
Akihutubia ufunguzi wa kongamano hilo waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi, amesema suala la makundi ya kigaidi kutumia fursa za utandawazi wa dunia na maendeleo ya teknolojia za upashanaji habari katika kueneza itikadi kali, limekuwa moja ya changamoto kubwa zinazotishia usalama wa kimataifa, na ugaidi kwenye mtandao wa Internet, pia limekuwa chanzo kikuu kinachochochea ongezeko la shughuli za kigaidi katika miaka ya hivi karibuni kote duniani.
"Ugaidi kwenye mtandao wa Internet unawarubuni watu, na kuzifanya itikadi kali zienezwe kwa urahisi zaidi kuliko wakati wowote ule, ugaidi wa aina hiyo unatumia mbinu za kisiri kupitia mtandao kwa ajili ya kupunguza gharama na ugumu wa kiufundi wa kuendesha shughuli za kigaidi, na vilevile kuinua uwezo wao wa kufanya shughuli hizo. Ugaidi kwenye mtandao umevuka mipaka ya nchi na kuamsha makundi mbalimbali ya kigaidi kote duniani yaliyojificha na kusubiri fursa, hali ambayo imeharakisha muungano wa nguvu za kigaidi duniani."
Bw. Wang Yi amesisitiza kuwa China ikiwa ni mshiriki na mtoa mchango katika shughuli za kupambana na ugaidi duniani, inapinga kithabiti ugaidi wa aina zote, na inajitahidi kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika eneo hilo. Bw. Wang Yi ameeleza mapendekezo matatu ya China.
"Kwanza, bila kujali ni mapambano dhidi ya ugaidi katika vita halisi au kwenye mtandao wa Internet, nchi mbalimbali zinapaswa kushirikiana kwa pamoja chini ya mtizamo wa kuwa wanachama wa Jumuiya yenye hatma ya pamoja; Pili, tunapaswa kusukuma mbele ushirikiano hatua kwa hatua. Jumiya ya kimataifa imefikia makubaliano kuhusu hatari na madhara ya itikadi kali, na inaweza kutoa kipaumbele katika ushirikiano wa kupambana na video na sauti zinazoeneza itikadi kali kwenye mtandao, na kwenye msingi huu tunaweza kujadili na kutunga kwa pamoja mwongozo wa ushirikiano wa kupambana na ugaidi kwenye mtandao wa Internet. Tatu, tunapaswa kukusanya wataalamu bingwa, kuongeza nguvu katika uvumbuzi wa kiteknolojia, na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa kwenye vita hivyo, ili kufichua na kuangamiza shughuli zote za kigaidi kwenye mtandao wa Internet."