Update:

21 October 2016

Bunge laigomea Serikali kisa posho

Athari za kutokuwepo kwa posho za safari za wabunge zimeanza kuonekana baada ya ripoti kuhusiana na mazingira kugomewa na wabunge na hivyo waziri husika kukosa fursa ya kwasilisha ili kujadiliwa

Tukio hilo lililoshuhudiwa na waandishi wa habari lilijitokeza mjini Dodoma jana, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, kukataa kujadili taarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kuhusu utupaji wa taka sumu katika maeneo ya migodi ya madini na pia bomoabomoa kwenye maeneo ya mabondeni.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walisema hawawezi kujadili taarifa hiyo wakati hawajawahi kufika kwenye maeneo husika kujionea uhalisia na kwamba, wanachoona ni kuwa hatua za kubana matumizi ya Serikali zinasababisha Bunge kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yake kwa ufanisi.
Kamati hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, aliyefuatana na wataalamu wake, kuingia katika kikao cha kamati ili kuwasilisha taarifa hiyo.
Hata hivyo, kabla ya taarifa hiyo kuwasilishwa, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Vicky Kamata, alisema kuwa kabla ya kuwasilishwa, ni vyema akaruhusu wajumbe kuzungumza machache kuhusu taarifa hiyo.
Alisema kamati inataka ijue tatizo ni nini kwa sababu tangu waanze kufanya kazi na wizara hiyo, hawajawahi kufika kwenye maeneo husika na hawako tayari kujadili kinadharia.
Baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza, ndipo Mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Laizer, alipoeleza kuwa kwa maoni yake, Serikali inajificha katika kivuli cha kubana matumizi kulinyima Bunge kutekeleza majukumu yake.
Laizer alisema amekuwa akisikia migodi ina maji yenye sumu yanatiririka kwa wananchi lakini kamati haijawahi kufika kwenye mgodi hata mmoja kati ya migodi tisa iliyokuwa kwenye taarifa hiyo ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Alisema taarifa hiyo haitajadiliwa hadi Serikali na Bunge watakapokuwa na fedha kwa ajili ya wabunge kufanya ziara kujionea uhalisia na ndipo wapate cha kujadili.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Anatropia Theonest, alisema: "Kama Serikali inabana matumizi, hakuna umuhimu wa kuwapo kwa kamati… ni vyema (kamati) zikaondolewa kwa kuwa zinashindwa kutekeleza majukumu kwa mujibu wa katiba."
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Tauhida Galoss Nyimbo, alisema ni vyema Serikali ikatambua kamati inafanya kazi kwa maslahi ya wananchi na si kwa maslahi ya wizara na serikali.
Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji, alisema wabunge wanapaswa kujua kwa undani maeneo hayo kwa kufanya ziara na kujionea uhalisia na kwamba suala la mazingira ni gumu na endapo watapokea taarifa hiyo na kuijadili, watakuwa wamepokea kutoka upande mmoja badala ya kujua ukweli wa hicho wanachotakiwa kukiijadili.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Hawa Mwaifunga, alisema: “Taarifa nimeisoma… lakini wakati naisoma, nikajisikia kizunguzungu maana sina uelewa na hayo mambo. Sisi hatuwezi kukubali kujadili taarifa wakati hatujui hali halisi kule. Mbona mawaziri wanafanya ziara?
"Inashindikanaje kuchukua hata wabunge watatu waambatane (wafuatane) nao ili wajue kinachoendelea?”
Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Mussa Sima, Mbunge wa Singida Mjini (CCM), akieleza kuwa taarifa waliyopewa iko kinadharia zaidi na wabunge hawawezi kufanyia kazi picha kwa kuwa watakuwa wanawahadaa Watanzania.
KAULI YA SERIKALI
Kutokana na mgomo huo wa wabunge, Naibu Waziri Mpina, aliigeuzia kibao kamati kwa kudai kuwa amekuwa akishangazwa na utendaji wake huku akihoji sababu za kutoitembelea wizara yake.
Mpina ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo (kipindi hicho ikiitwa Kamati ya Viwanda, Uchumi na Biashara), alisema suala la ziara si jukumu la wizara bali kamati ina wajibu wa kusema na kupanga inataka kwenda maeneo gani kupitia kwa Katibu wa Bunge.
Alisema Katibu wa Bunge ana fungu kwa ajili ya ziara za kamati na ikitokea akakosa fungu, anaweza kuwasiliana na wizara kuangalia uwezekano wa kuwezesha suala husika.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Peter Kafumu, alisema safari iliyopita walijaribu kuomba, lakini walikutana na vipingamizi vingi pamoja na wizara kuonyesha nia ya kusaidia ili waende walikotaka kwa nia ya kutekeleza majukumu yao.
KAULI YA SPIKA
Alipotafutwa na Nipashe kwa simu jana kuzungumzia suala hilo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema: "Tunalichukua suala hili kama changamoto na tutalifanyia kazi."
MABILIONI YALIVYOFYEKWA
Juni mwaka huu wakati wa Bunge la Bajeti, ilibainika kuwa Bunge ni miongoni mwa taasisi ambazo zimekumbwa na mpango wa serikali wa kubana matumizi kutrokana na kufyekwa kwa bajeti yake ya mwaka huu wa fedha (2016/17).
Taasisi nyingine ambazo bajeti zake zimefyekwa kwa takribani asilimia 60 kulinganishwa na mwaka wa fedha 2015/16, ni pamoja na Mahakama na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (fungu la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG).
MFUKO WA BUNGE
Bajeti ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2015/16 ilikuwa Sh. bilioni 173, lakini wakati wa mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha, ilibainika chombo hicho cha kutunga sheria kimetengewa Sh. biloni 99.066 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake, ikiwa ni punguzo la Sh. bilioni 73.934 (asilimia 42.7).
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kati ya fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya Bunge, Sh. bilioni 92.066 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati miradi ya maendeleo imetengewa Sh. bilioni saba.
BILIONI 6/- KUREJESHWA
Wakati wabunge katika kamati ya Dk. Kafumu wakilalamikia kukosa fedha za safari, hivi karibuni uongozi wa Bunge ulirejesha Sh. bilioni sita serikali ulizodai kuziokoa kutokana na kubana matumizi katika mwaka uliopita wa fedha.
Katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali itatumia Sh. trilioni 29.53. Kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 17.72 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 11.82, sawa na asilimia 40 ya bajeti. zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo.