Update:

08 September 2016

Kiama: wenye vyeti feki kutumbuliwa ama kuburuzwa mahakamani .

Ni dhahiri sasa kwa watumishi wa Umma ambao walipata ajira kwa kutumia vyeti feki wanasubiri kutumbuliwa kwenye nafasi zao ama kuburuzwa mahakamani pengine kuanzia mwezi huu

Hali hiyo imebainika baada ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk. Charles Msonde kuiambia Nipashe jana wamemaliza uhakiki kwenye baadhi ya taasisi na kukabidhi taarifa za vyeti vilivyogundulika kuwa feki kwa waajiri ili wachukue hatua stahiki.

Dk. Msonde alisema kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma, wafanyakazi wanaopatikana na vyeti vya kughusi ama kutumia vya watu wengine ili kupata ajira, hatima yao ni kufukuzwa kazi na kushtakiwa.
Mahojiano na mwandishi wa habari hizi  yalikuwa hivi:
Swali: Mpaka sasa ni watu wangapi mmebaini kwamba wanatumia vyeti feki?
Jibu: Ni mapema mno kutamka idadi; kwa sasa baraza haliwezi kusema idadi kwa sababu kazi ndio kwanza imeanza kwa sababu wanaohakikiwa ni wafanyakazi wa nchi nzima na ni wengi.
Kusema idadi sasa hivi siyo sahihi kwa sababu tumefanya kwenye halmashauri chache na taasisi chache. Yatosha tu kusema kwamba tunapofanya uchunguzi tunabaini uwepo wa wafanyakazi wachache waliotumia vyeti feki ama wametumia vyeti vya watu wengine. Na hao wanaondolewa mara moja kwenye mfumo wa ajira kila tunapowabaini.
Swali: Kati ya taasisi mlizochunguza, ipi yenye vyeti vingi feki?
Jibu: Nimeshasema ni mapema mno kwa sasa, kwa mfano tumechunguza taasisi ya Mamlaka ya Bandari (TPA), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, baadhi ya halmashauri, Muhimbili na kwingineko. Kwa hiyo ndiyo maana nasema itakapofika wakati mwafaka tutatoa uchambuzi wa taasisi kwa taasisi, halmashauri kwa halmashauri.
Swali: Mliowapata wakitumia vyeti hivyo wameshawachukuliwa hatua?
Jibu: Kazi yetu sisi ni kufanya uhakiki tukishamaliza tunamwambia mwajiri achukue hatua kwa mujibu wa kanuni za utumishi, na hatua zinazochukuliwa kwa vyovyote ni kumwachisha kazi na kumfungulia mashtaka.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, aliliambia gazeti hili kuwa amepata taarifa za baadhi ya wafanyakazi kuacha kazi wenyewe kufuatia uhakiki huo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, wafanyakazi wengine wanaendelea na kazi huku wakisubiria kujua hatima yao.
“Zipo taarifa za watu kuacha kazi na wengine wanasubiria kujua hatima yao… kwa sasa ni vigumu kujua ni wangapi walioacha kazi kwa kuwa tunaendelea na uhakiki wetu,” alisema Dk. Ndumbaro.
Awali serikali ilitangaza rasmi kuanza kwa kampeni ya kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wote walioajiriwa wakitumia vyeti bandia.
Aidha, watumishi hao walitakiwa kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya kufikiwa na mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi wa umma yanayokuja nchini.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma wakati wa majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako alisema serikali imedhamiria kuboresha kiwango cha elimu nchini na kwamba, hatua mojawapo inayochukuliwa sasa ni kukagua uhalali wa vyeti vyote vya elimu kwa watumishi wa umma katika sekta ya elimu na sekta nyinginezo.
Kutokana na agizo hilo hofu zaidi inadaiwa kujitwalia miongoni mwa watumishi walioingia kwenye mfumo wa ajira za serikali kupitia ‘vimemo’ kutoka kwa wakubwa na pia matumizi ya vyeti bandia.
Katika sakata hilo wapo vigogo ambao wanadaiwa kughushi vyeti vyao ambapo walikuwa wakihaha baada ya kusikia taarifa hiyo.
Baada ya kutangazwa kwa operesheni hiyo, ilibainika kuongezeka ghafla kwa matangazo ya kupotea kwa vyeti vya elimu katika vyombo mbalimbali vya habari huku wengine wakitangaza kupotolewa na vyeti mpaka viwili, kikiwamo cha kidato cha nne na cha sita.
source:ippmedia.com