Update:

09 September 2016

Chanzo cha ajali msafara wa Samia ni hiki

Mwendo kasi umeelezwa kuwa ndio chanzo cha ajali ya moja ya magari yalio kuwa kwenye msafara wa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan lililo pata ajali katika kijiji Nanguruwe mkoani Mtwarwa


Imeelezwa kuwa dereva wa gari hilo, alishindwa kulimudu na kuacha njia hivyo kwenda porini na kusababisha watu watano kujeruhiwa. Msafara huo ulikuwa ukitoka Ikulu ndogo ya Mtwara kwenda wilayani Tandahimba, mkoani humo.
Ajali hiyo iliwajeruhi vibaya dereva wa gari hilo na wasaidizi wanne wa Makamu wa Rais.
Kabla ya kutokea ajali hiyo, gari lililokuwa limebeba waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, nalo lilinusurika kupinduka katika eneo hilo, baada ya kuacha njia.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema gari hilo lilipinduka na kusababisha watu hao kujeruhiwa.
Alilitaja gari hilo kuwa ni aina ya Toyota Landcruiser V8, lenye namba za usajili ST 244 A .
Dendego alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na kwamba wamewapeleka Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Ligula kwa ajili ya uangalizi wa madaktari.
“Gari limepata madhara na watu wameumia ila niwatoe tu hofu, majeruhi wote hawajambo isipokuwa tumewapeleka hospitali ya Mkoa kwa ajili ya uangalizi na msafara unaendelea,” alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema watu wengine walioko kwenye msafara huo wa Makamu wa Rais wako salama na wameendelea na ziara kwenda wilayani Tandahimba.
Samia alianza ziara ya kikazi mkoani Mtwara Septemba 7, mwaka huu, ambayo itamalizika leo. Mojaya shughuli alizofanya ni kuzindua jengo la Sekrtarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Kusini lililoko mjini Mtwara.
Pia alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha kuchakata gesi katika kijiji cha Madimba, wilaya ya Mtwara.