Update:

29 August 2016

Yanga yarejea ‘anga’ zake


Bao la kwanza la mabingwa hao lilifungwa na Deus Kaseke katika dakika ya 18, aliyemalizia kazi nzuri iliyofanywa na Hassan Kessy huku mabeki wa African Lyon wakitegeana wakidhani mchezaji huyo ameotea.
Simon Msuva alifunga bao la pili kwa Yanga, baada ya kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na Thaban Kamusoko na kuwazidi mbio mabeki wa African Lyon na kumpiga chenga kipa wao, Youthe Rostand, na kufunga kirahisi.
Akiingia kuchukua nafasi ya Msuva, straika Juma Mahadhi alifunga bao la tatu katika dakika ya 90 kwa shuti kali la mita 26 lililomshinda kipa wa African Lyon, Rostand, kudaka na kujaa wavuni moja kwa moja.
Mechi hiyo ilianza kwa kasi huku kila upande ikionekana ikicheza kwa ‘mahesabu’ na kushambuliana kwa zamu, lakini hadi wanakwenda mapumziko, Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0.


African Lyon walikaribia kupata bao kupitia kwa Tito Okello, lakini mpira wake wa kichwa alioupiga katika dakika ya nane ulidakwa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’, na kuikosesha timu hiyo bao la mapema.Katika mechi nyingine iliyochezwa jana ya ligi hiyo Mbeya City ilifanikiwa kuondoka na pointi tatu dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza, baada ya mchezaji wake Haruna Shamte kuifungia bao kwa njia ya frikiki katika dakika ya saba.


Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’ , Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Vincent Andrew ‘Dante’, Vincent Bossou, Simon Msuva/ Juma Mahadhi (dk 76), Haruna Niyonzima, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma/ Anthony Matheo (dk 88), Amissi Tambwe na Deus Kaseke.


African Lyon : Youthe Rostand, Khalfan Twenye, Hamad Tajiri, William Otong, Omary Salumu, Aman Peter, Mussa Nampaka, Bakari Jaffari, Omary Abdallah/ Mussa Nampaka (dk 75), Hood Mayanja na Tito Okello.