Update:

01 August 2016

Watu 500 wakamatwa kwa kutodai risiti

Mamlaka ya mapato nchini (TRA) imesema zaidi ya watu 500 mikoa mbalimbali nchini wamekamatwa  na kutozwa faini kutokana na kununua bidhaa na kuacha kutoa risiti

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema gharama ya faini iliyotozwa kwa watu hao bado haijafahamika kwa sababu bado majumuisho kwa nchi nzima yalikuwa hayajakamilika.
Kayombo alisema pia kwamba ndani ya mwezi mmoja, matumizi ya mashine za kielektroniki za kutoza kodi (EFD), yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 27.
Pia alisema kwamba baada ya Julai 31 (juzi), wangeanza kukusanya takwimu kwa nchi nzima na kisha kutoa taarifa rasimi.
“Kwa sasa hivi ni vigumu kupata takwimu halisi ya faini waliyotozwa, subiri wiki moja ipite naweza kukujulisha kiasi cha fedha tulichokipata kwa wateja walionunua bidhaa bila kudai risiti,” alisema Kayombo.
Kayombo aliwataka wananchi kuhakikisha wanapokwenda kununua bidhaa wahakikishe wanadai risiti la sivyo watachukuliwa hatua ikiwamo kulipa faini.
“Kila mwananchi anapokwenda kununua bidhaa ahakikishe anadai risiti bila kufanya hivyo tutamlipisha faini ama kumfikisha mahakamani wapo ambao tumewafikisha mahakamani,” alisema Kayombo.
Akizungumzia kuongezeka kwa mashine za EFD kwa asilimia 27, alisema wafanyabiashara wanatakiwa kuzitumia mashine hizo wanapouza bidhaa zao ili serikali ipate mapato na atakayekiuka kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya kupitishwa kwa sheria kali kuwabana wasiotumia mashine hizo EFDs, wafanyabiashara walikuwa wakiendesha migomo wakipinga mashine hizo kutokana na kile walichosema zinawapunja.
Baada ya kuingia madarakani, Rais John Magufuli, aliishauri TRA kutoa mashine hizo bure ili kukusanya kodi.
Pia kwenye kikao kilichopita cha Bunge la Bajeti, lilipitisha sheria ya kumbana mteja ambaye anashindwa kudai risiti anaponunua bidhaa husika, ambapo anapokamatwa atatakiwa kutozwa faini ama kifungo.