Update:

16 August 2016

Siri mkataba wa Lugumi sasa kuanikwa hadharani

Siku moja baada ya Spika wa bunge Job Ndugai kutangaza mkataba tata kampuni ya Lugumi Interprises Limited na jeshi la polisi litajadiliwa mwezi ujao mjini Dodoma kamati ya kudumu ya bunge ya hesabu za serikali PAC imesema imepata nguvu ya kuliweka wazi zaidi kwa umma


Aidha, PAC imesema leo inakaa kuandaa ripoti ambayo itaiwaiwasilisha katika mkutano ujao huo wa bunge.
Katika mahojiano na kituo cha Azam televisheni jijini Dar es Salaam juzi, Ndugai alisema sakata hilo litajadiliwa katika mkutano wa Bunge utakaoanza Septemba 6.
Kampuni hiyo ilikuwa inatekeleza mradi wenye thamani ya Sh. bilioni 37 wa kusimika mfumo wa utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchi nzima.
Katika mahojiano na Nipashe jana, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilary, alisema kuwa kutokana na uzito wa suala hilo, leo wanaanza kukaa kuandaa ripoti ambayo wataiwasilisha bungeni ili wananchi wafahamu ambacho kamati ndogo ya PAC ilikibaini baada ya kutembelea vituo vya polisi ambavyo mfumo huo ulikuwa unasimikwa.
"Tamko la Ndugai limetupa nguvu ya kuueleza umma yale tuliyoyabaini. Kamati ina maazimio yake tutayaweka wazi kwa umma wakati wa vikao vya mkutano ujao wa bunge," Hilary alisema.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa maelezo kuwa si msemaji wa kamati, alisema walibaini 'uozo' katika utekelezaji wa mradi huo lakini walikosa nafasi ya kuueleza baada ya bunge kutoa tamko na kuifanya kamati ionekane haina meno.
"Kamati ilikosa nafasi ya kuueleza umma ilichokibaini baada ya Dk. Tulia Ackson kutoa tamko la bunge kuhusu mradi huo,"
alisema mjumbe huyo.
Juni 30 wakati wa kuliahirisha bunge, Dk. Ackson aliitaka serikali kukamilisha mradi huo ndani ya miezi mitatu kuanzia siku hiyo.
Hilary ambaye pia ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), alisema kamati ilikuwa imepanga kupitia ripoti za hesabu mbalimbali za mashirika ya umma lakini italazimika kupangua ratiba yake ili kukamilisha ripoti ya sakata hilo.
Aprili 23, PAC iliunda kamati ndogo ya watu tisa iliyoongozwa na mwenyekiti Japahet Hasunga ambaye ni mbunge wa Vwawa (CCM), ili itembelee vituo vya polisi Tanzania Bara na visiwani kuchunguza utekelezaji wa mradi huo.
PAC ililazimika kuunda kamati hiyo ndogo baada ya kushindwa kupata ufafanuzi wa kina kutoka kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira na maofisa wengine wa Jeshi la Polisi iliyowahoji kwenye ofisi za Bunge Aprili 20 kuhusu sakata hilo.
Baada ya kumaliza uchunguzi wake, kamati ndogo ya PAC yenye wajumbe (wabunge) watano wa CCM na wanne kutoka upinzani (vyama vya CUF na Chadema vikitoa wajumbe wawili kila kimoja), ilirejea bungeni mjini Dodoma Mei 24.
Mwanzoni mwa Aprili, PAC ilieleza kuwa kampuni ya Lugumi ililipwa Sh. bilioni 34 na Jeshi la Polisi ili kufunga vifaa hivyo katika vituo 138 vya polisi nchini, lakini ni vituo 14 tu ndivyo vilivyokuwa vimefungiwa, licha ya kulipwa fedha hizo ambazo ni sawa na asilimia 90 ya malipo yote ya kazi hiyo.
Ulipaji wa asilimia 90 ya malipo ya kandarasi kabla ya kukamilika kwa kazi ni kinyume na sheria ya manunuzi ya umma.