Update:

19 August 2016

Sheria kali ya kuwabana wavuta sigara ovyo yaja

Serikali imesema kwamba inatarajia kutunga sheria kali kwa wavutaji wa sigara hadharani

Imesema hatua hiyo inatokana na idadi ya wavutaji nchini kuongezeka kwa kasi na kufikia asilimia 27 huku wakazi wa Dar es Salaam wakiwa vinara.
Kutokana na idadi ya wavutaji kuongezeka, serikali huingia hasara ya Dola milioni 136 (Sh. bilioni 291.37) kwa ajili ya kuwatibia waathirika wa uvutaji wa sigara, kwa mujibu wa utafiti wa Hospitali ya Taifa Muhimbili uliofanywa mwaka 2014.
Vilevile, idadi ya watu wanaofariki dunia kwa uvutaji wa sigara duniani kwa mwaka imefikia 600,000, na kwamba kati ya idadi hiyo, 430,000 ni watoto asilimia 64 wakiwa ni wa kike.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mkutano na wadau wa afya kutafuta namna bora yambinu za kudhibiti matumizi ya tumbaku.
Alisema asilimia 27 ya wananchi Tanzania, huvuta sigara, kati ya idadi hiyo, wanaume ni asilimia 24 na wanawake ni asilimia 2.6.
“Kuna haja ya kupeleka sheria kali bungeni ili ipitishwe kwa wavutaji wa sigara hadharani, haiwezekani watu wanavuta hadharani na kuwasababishia madhara watu wengine,” alisema Waziri Mwalimu.
Aliongeza kuwa kuanzia Oktoba mosi, mwaka huu, serikali itaanza kukamata sigara zote zisizo na onyo la `Uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako.'
Alisema sambamba na hilo, pia itaanza kuwakamata wauzaji wa sigara wanaowauzia watoto wenye chini ya umri 18.
Alisema Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa wananchi wake kuvuta sigara kwa asilimia 10.9, ukifuatiwa na Arusha asilimia 10.6 na Kilimanjaro asilimia 7.6.
Waziri Mwalimu alisema uvutaji sigara nchini unaongezeka kila mwaka na kwamba katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na Muhimbili, kati ya wagonjwa 100 wanaokwenda kutibiwa hospitali hizo, wagojwa 32 wameathiriwa na uvutaji sigara.
Alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni sita hufariki dunia kila mwaka kutokan na uvutaji sigara huku wengi wao wakiwa ni vijana wenye umri wa kuanzia miaka 30 hadi 69.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Uboreshaji Afya, Hellen Semu, alisema duniani watu wanaokadiriwa milioni 5.8 hufariki dunia kwa mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku.
Alisema kati ya hao, asilimia 22 hupata magonjwa ya kansa, asilimia 71 kansa ya mapafu na kwamba endapo matumizi ya tumbaku yakiendelea, idadi ya vifo vya watu duniani vitokanavyo na matumizi ya tumbaku, itaongezeka na kufikia milioni nane ifikapo mwaka 2030.