Update:

16 August 2016

Seif ataja serikali 3 mazishi ya Jumbe

Katibu wa chama cha wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad Amesema wazo la Rais wa zamani wa  Zanzibar Aboud Jumbe la kutaka kuanzishwa kwa mfumo wa serikali tatu kwenye Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lilikuwa mwafaka lakini hakushirikisha wenzake wakati huo

Akizungumza kwenye mazishi ya Jumbe yaliyofanyika jana mchana nyumbani kwa marehemu Migombani, Zanzibar, Maalim Seif aligusia kilichochangia kumwondoa Jumbe madarakani mwaka 1984.
Jumbe alifariki dunia juzi nyumbani kwake eneo la Mji Mwema, Kigamboni jijini Dar es Salaam baada ya kuugua muda mrefu.
Alijiuzulu nyadhifa zake zote mwaka 1984 baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) kilichofanyika Januari 30, mjini Dodoma.
Jumbe aliachia ngazi kama Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM katika kile kilichodaiwa kuchafuka hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar.
Pia Waziri Kiongozi wake, Ramadhan Haji Faki, naye alilazimika kujiuzulu.
Hata hivyo, ilikuja kujulikana kuwa baadae kuwa alikuwa ameandaa mkakati wa siri wa kushinikiza kisheria kuanzishwa kwa mfumo wa serikali tatu kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maalim Seif akiwa Mjumbe wa NEC wa CCM wakati huo, anatajwa kuwa ndiye aliyevujisha siri ya mpango huo kwa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, wakati huo.
Akizungumzia suala hilo ingawa siyo kwa undani, Maalim Seif alisema msimamo wa serikali tatu ndiyo msimamo wa CUF katika kutafuta mamlaka kamili ya Zanzibar, lakini alishindwa kumuunga mkono Jumbe wakati huo kwa sababu hakuwashirikisha viongozi wenzake wakati huo.
Maalim Seif, hata hivyo, alisema kuwa wazo la Jumbe limeendelea kupiganiwa na wapinzani kwa madhumuni ya kutaka mamlaka kamili ya Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hata hivyo, alimsifia Jumbe kwa kuwaunganisha wazanzibari wakati wa uongozi wake kabla ya kujiuzulu mwaka 1984.
Alisema kuwa serikali awamu ya pili chini ya uongozi wake alifanikiwa kuwaingiza watu wenye asili ya Pemba katika baraza lake la mawaziri na nafasi nyingine na kuondoa dhana ya wapemba kubaguliwa katika serikali.
“Uongozi wake ulifanikiwa kuwaunganisha wazanzibari baada ya kuunda Baraza la Mawaziri likiwa na watu kutoka Pemba na Unguja kinyume na siku za nyuma baada ya Mapinduzi kufanyika Zanzibar,”alisema Maalim Seif.
Alisema kuwa ameguswa na msiba wa Jumbe na kuamua kuhudhuria mazishi yake kwani alikuwa mwalimu wake na mtu mwenye mchango mkubwa katika safari yake ya maisha ya kisiasa visiwani humo.
“Alinichagua kuwa katibu wake nikiwa mwalimu, kabla ya kuniteua kuwa Waziri wa Elimu, na sisi ndiyo wanafunzi wa kwanza wa Zanzibar tuliopelekwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” alieleza Maalim Seifa.
Maalim Seif alisema Jumbe alikuwa kiongozi mwenye msimamo na alitetea mtazamo wake wa kuwa na muungano wa serikali tatu bila ya kuyumba hadi mwisho wa uhai wake.
Maalim Seif alisema msimamo wa serikali tatu ndiyo msimamo wa CUF katika kutafuta mamlaka kamili ya Zanzibar lakini alishindwa kumuunga mkono wakati huo kwa sababu hakuwashirikisha viongozi wenzake wakati huo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Fedha wa zamani wa Serikali ya Muungano Abdulsalam Isssa Khatibu ametofautiana na Maalim Seif akidai kuwa wazo la Jumbe la serikali tatu halikuwa lake binafsi bali lilikuwa linaungwa mkono na wananchi walio wengi.
Khatibu alisema wazo la Jumbe la kuwa na Muungano wa serikali tatu halikuwa wazo lake binafsi mwaka 1984 bali ni mkusanyiko wa fikra za wananchi walio wengi kwa wakati ule visiwani Zanzibar.
Alisema kuna wananchi wengi walikuwa wakitaka mabadiliko yafanyike katika mfumo wa muungano lakini kulikuwa na wanasiasa wasaliti wa fikra hizo wa Zanzibar na kuwa chimbuko la Mzee Jumbe kufikia hatua ya kuvuliwa wadhifa wake na chama.
Alisema Jumbe alikuwa na msimamo na ndio maana hakuyumba katika wazo lake la kuwa na muungano wa serikali tatu pamoja na kupoteza wadhifa wake kinyume na wanasiasa wengine Zanzibar.
Khatibu alimpiga kijembe Maalim Seif akidai kuwa wanasiasa waliokuwa wakipinga wazo la kuwa na muungano wa serikali tatu wakati ule ndiyo walewale baadhi yao sasa wanataka serikali tatu.
“Jumbe kabla ya kufa kwake ameshuhudia walewale waliokuwa wakimpinga na kumuacha kumuunga mkono leo wakitaka yaleyale ambayo alikuwa akipigania,” aliongeza Khatib.
Khatibu alisema baadhi ya wanasiasa walimtuhumu Jumbe kuwa alikuwa anatengeneza mazingira ya kubakia madarakani maisha na wengine wakidai alikuwa anataka kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.