Update:

17 August 2016

Sare za polisi zawaponza kina `Masanja Mkandamizaji' ,Joti

Jeshi la Polisi kanda maalumu jijini Dar es salam limesema litachukua hatua kali dhidi ya kundi la kisanii la 'Original Comed kutokana na kuvaa mavazi  yanayo shabihiana na sare za jeshi la polisi


Mwishoni mwa wiki, kundi hilo lilivaa nguo hizo wakati wa mapokezi ya harusi ya Emmanuel Mgaya 'Masanja Mkandamizaji', mmoja wa wasanii wa kundi hilo.
Katika taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Bulimba, ilieleza kuwa jeshi hilo halitamvumilia mtu yeyote anayefanya kitendo hicho na litachukua hatua za kisheria dhidi ya wasanii hao.
"Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza tabia kwa baadhi ya watu wakiwamo wasanii, watu wengine na mmoja mmoja kutumia mavazi yanayofanana na sare za majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini likiwamo Jeshi la Polisi katika shughuli zao za kisanii au katika kazi mbalimbali, jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa sheria ya kanuni za makosa ya jinai, sura ya 16 na marejeo yake ya mwaka 2002, kifungu cha 178(1) na (2) vinavyozungumzia makosa dhidi ya sare za majeshi ya ulinzi na usalama, kinabainisha wazi kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama kuvaa mavazi yanayotumiwa au kushabihiana na sare za majeshi hayo bila kibali kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wale wote wenye mavazi yanayoshabihiana na sare za majeshi ya ulinzi na usalama kuzisalimisha mara moja katika vituo vya polisi vilivyo karibu nao," ilieleza zaidi taarifa hiyo.