Update:

01 August 2016

Mrema awapa siku 7 polisi wala rushwa


Mwenyekiti wa bodi ya Parole Augustine Mrema amewapa siku saba madera wa pikipiki za kupakia abiria maarufu kama "bodaboda" wa wilaya ya kinondoni kumpelekea majina ya askari wa jeshi la polisi wanao omba rushwa ili ayapeleke kwa Rais Magufuli


Mrema aliyasema hayo jana alipokutana na Chama cha waendesha bodaboda na bajaji wa wilaya ya Kinondoni ambapo walimweleza kuwa, moja ya kero inayowakabili ni kuombwa rushwa na polisi.
Baada ya kuelezwa jambo hilo, Mrema alijibu: “Si mnawajua polisi wanaowaomba rushwa, sasa nataka muwaandike katika karatasi majina yao ndani ya siku saba, namba yake hata ikiwekezekana mpigeni picha, halafu mniletee ofisini kwangu ili nianze nao kazi.”
Kuhusu bodaboda kutoingia mjini, Mrema alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutoa maelezo ya kutosha kuhusu hali hiyo wakati eneo la Posta kuna kituo cha madereva wa bodaboda.
“Ndani ya siku saba, nitazifuatilia zile bodaboda zilizopaki kituo kilichopo karibu na kituo cha mafuta kilicho karibu na Ofisi za Posta katikati ya Jiji ili nijue ni za nani? Na kwa nini zinapaki mjini wakati kuna zuio,” alisema Mrema.
Mrema pia aliwataka madereva bodaboda wote nchini kutokubali kutumiwa na wanasiasa wakati wa maandamano wala wakati wa uchaguzi, bali wajielekeze katika kufanya kazi za maendeleo.
Alisema uchaguzi mkuu ulishamalizika na kilichobakia kwa sasa ni kumsaidia Rais Magufuli katika kuleta maendeleo ya nchi kwa kuwa yeye ndiye Rais na hakuna mtu mwingine.
Mrema alisema ameanza kutatua kero za waendesha bodaboda kwa sababu amepewa kazi ya kuongea na vijana ili kuondoa makosa ambayo yatawafanya kupelekwa mahabusu.
Alisema kwa sasa vijana wanakamatwa ovyo na kupelekwa vituo vya polisi na mwishowe kupelekwa mahakamani na kuhukumiwa na kwamba hali hiyo inaongeza idadi ya mahabusu.
Akielezea sababu iliyomtoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia NCCR-Mageuzi, Mrema alisema uwapo wa ufisadi ndani ya chama hicho miaka ya 1990, ndiyo sababu pekee iliyomkimbiza.
“Nilimwambia Lowassa wakati huo kuwa `maji yameshachemka weka unga tusonge ugali,’ lakini hakunisikia yeye na mwenzake Sumaye, matokeo yake mwaka 2008, akajiuzulu baadaye nikasikia amekatwa, leo yupo upinzani na Sumaye, angenisikiliza wakati ule haya yote yasingemkuta,” alisema Mrema.
Mrema wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuanzia mwaka 1990 hadi 1994, alisifika kwa utoaji wa maagizo ya kutaka mambo kufanyika kwa siku saba.