Update:

10 August 2016

Mbowe, Lissu wahofia ubunge wao

Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA)na mwanasheria  Freeman Mbowe wa chama hicho Tundu Lissu wamelazimika kujibu barua walio tumiwa na secretariti ya maadili ya utumishi wa umma wakiofia kuvuliwa ubunge wao

Wawili hao wametakiwa kujieleza kwa sekretarieti hiyo ndani ya siku 21 kuanzia Agosti 4, mwaka huu kuhusu kile ambacho Lissu alikieleza jana kuwa ni tuhuma za kuhusika kwao katika kosa la kukiuka masharti ya hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.
Licha ya kuikosoa barua aliyotumiwa na sekretarieti hiyo, viongozi hao wa Chadema ambao pia ni wabunge, Mbowe Jimbo la Hai na Lissu (Singida Mashariki), watalazimika kuijibu kwa kuwa wamebaini ni huenda kuna njama inayofanywa kuwavua ubunge wao.
Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alisema kuwa katika barua hiyo aliyodai imeandikwa na Kamishna wa sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Salome Kaganda, inaelezwa kwamba viongozi hao wamekiuka masharti ya hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa kutoa matamshi yanayochochea wananchi kutotii sheria.
Alisema sehemu ya barua hiyo ilieleza kuwa matamshi hayo yanatokana na maazimio yaliyofikiwa na kikundi cha watu wachache nje ya Bunge, yakipuuza utengamano, utulivu na usalama wa wananchi wengine kinyume cha dhana ya maslahi mapana ya umma.
Dk. Mashinji alisema walishtuka baada ya kupokea barua hiyo na hawakuamini kama imendikwa na Jaji kwa kuwa “haikuwa na maelezo yoyote ya kile kinachodaiwa kosa, haikutaja tarehe ya kufanyika kwa kosa hilo, muda au mahali kosa lilipotendeka.”
Katibu Mkuu huyo pia alisema haikutaja vifungu vya sheria yoyote iliyokiukwa au kuonyesha kama sekreterieti ya maadili ya viongozi wa umma ina mamlaka ya kisheria ya kushughulikia kosa hilo na kwamba barua hiyo ilionyesha upungufu wa kitaaluma na kiuandishi.
Akizungumzia barua hiyo, Lissu aliyekuwa amefuatana na Dk. Mashinji, alisema kuwa kwa namna barua hiyo ilivyoandikwa, imedhihirisha wazi kuwa Jaji Kaganda hana sifa ya kuendelea na wadhifa wake huo kutokana na upungufu wake.
Alisema barua hiyo iliyoandikwa na Jaji Kaganda, ina ishara ya kuwapo kwa njama za kuwafungulia mashtaka viongozi hao wakuu wa Chadema katika Mahakama ya Maadili kwa lengo la kuwavua ubunge na kwamba njama hiyo wameibaini na wamejipanga kuikabili.
Lissu alisema barua hiyo inaweza kuwa mtego wa kuwatafutia vigezo vya kikatiba vya kukosa sifa ya kuwa wabunge kwa sababu wanaweza kuhesabiwa kuwa ni watovu wa nidhamu endapo watashindwa kutii agizo la Jaji Kaganda la kujibu barua yake.
“Mojawapo ya vigezo vya kikatiba vya mtu kukosa sifa ya kuwa ubunge ni pamoja na kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa nidhamu au kwa kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Kamishna wa Maadili ana mamlaka ya kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma na kuunda mahakama (tribunal),” alisema Lissu.
“Mahakama hiyo inaweza kusikiliza tuhuma hizo na kupeleka taarifa ya mashauri hayo kwa kamishna ambaye atapaswa kuwasilisha nakala za taarifa hiyo kwa Rais na Spika wa Bunge. Kamishna wa maadili ndiye atakayeitisha mahakama hiyo baada ya mashauriano na Mwanasheria Mkuu na Jaji Mkuu,” alieleza Lissu.
Alisema kuwa kwa kuzingatia mazingira hayo ya kisheria na mazingira ya sasa ya kisiasa kwa vyama vya upinzani, barua hiyo ina lengo la kutengeneza mazingira ya kisheria yatakayosababisha kuitishwa mahakama hiyo kwa lengo la kuwakandamiza viongozi hao.
Alisema Chadema imebaini njama hizo na haitakubali kunyamazishwa na kuruhusu ukandamizaji wa viongozi wake kwa kutumia kivuli cha maadili ya viongozi wa umma na kwamba wako tayari kupambana na njama hizo.
JAJI KAGANDA
Alivyotafutwa na gazeti hili jana ili kutoa ufafanuzi wa maelezo ya Lissu, Jaji Kaganda alisema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa Lissu ndiyo ameamua kusema hayo aliyosema.
“Yeye (Lissu) ndiye amesema na yeye ndiye msemaji, kwa hiyo, ‘I have nothing to do with Chadema or any political party (sina cha kufanya juu ya Chadema ama chama chochote cha siasa,” alisema Kaganda.